TRA yaokoa Sh38milioni

Kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini(TRA) Charles Kichele (aliyevaa kofia) akiangalia pombe kali za Shimha ambazo hazina stika, wakati wa ziara ya kukagua ufungaji wa mashine za stempu za kielektroniki kwenye viwanda bia na pombe kali.Picha na Michael Jamson

Muktasari:

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata katoni 10,786 za pombe kali zilizokuwa ziingizwe sokoni bila kulipiwa ushuru wa bidhaa


Mwanza. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata katoni 10,786 za pombe kali zilizokuwa ziingizwe sokoni bila kulipiwa ushuru wa bidhaa.

Pombe kali hizo aina ya Shimha Waragi zimekatwa na kamishna mkuu wa mamlaka hiyo, Charles Kichere wakati akifanya ukaguzi wa ufungaji wa mashine za mhuri wa kieletroniki (ETS) kwenye viwanda vya bia na pombe kali jijini Mwanza.

Huku akikitaja kiwanda cha Premidis kuwa ndio kinachotengeneza pombe hizo, Kichere amesema kipo maeneo ya Nyakato wilayani Nyamagana, kwamba kilitaka kukwepa kulipa ushuru wa Sh38.6 milioni.

“Baada ya kuanza kufanya ukaguzi tumebaini vitu hivi, mfano katika katoni moja, kuna baadhi ya chupa hazina stika za TRA,” amesema Kichere.

Amesema walipokuwa katika kiwanda hicho walikuta baadhi ya chupa zikiwa na stika za zamani ambazo hazitumii ETS.

Pia kamishna huyo amefanya ziara katika viwanda vingine vya Serengeti Breweries na Tanzania Breweries, vyote vya jijini Mwanza.

Ametoa wito kwa wamiliki wote wa viwanda vya kutengeneza bia na pombe kufunga mashine za ETS kabla ya Februari, 2019.