Tabora yaanzisha jukwaa la fursa za biashara na uwekezaji

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri,akimkaribisha Waziri wa Biashara na Viwanda, Joseph Kakunda katika Jukwaa la fursa za Biashara na Uwekezaji Mkoa Tabora.

Muktasari:

Waziri Joseph Kakunda apongeza hatua hiyo akisema matunda yake yatanufaisha mkoa huo na taifa kwa ujumla

Tabora.Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda ameupongeza mkoa wa Tabora kwa kuaandaa jukwaa la fursa za biashara na uwekezaji.

Amesema mkoa huo umefanya jambo zuri la kuandaa jukwaa hilo ambalo matunda yake yataunufaisha mkoa na taifa kwa ujumla.

Waziri Kakunda amesema kwa kujua umuhimu wa jukwaa hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndiye atakayelizindua.

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri kwa niaba ya wakazi wa mkoa wa Tabora amempongeza Kakunda ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Sikonge kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Amesema hiyo inadhihirisha imani kubwa aliyonayo Rais John Magufuli kwake na wananchi wa Tabora.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kwinga amewahakikishia usalama na mazingira mazuri ya biashara  wawekezaji wanaotaka kwenda kuwekeza kwenye wilaya hiyo.

Amesema wilaya yake inafaa kwa uwekezaji kwa kuwa ina barabara nzuri  na ina maeneo ya kutosha kwa ajili ya kilimo na viwanda.

Pia alisema wilaya hiyo imebarikiwa kuwa na vitalu vya utalii na mazao ya misiti ikiwamo asali inayosifika kwa ubora nchini.