Takukuru watakiwa kumchunguza mkurugenzi

Muktasari:

Mkuu wa mkoa wa Mara ameagiza taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumhoji mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime vijijini, huku katibu tawala wa mkoa huo akiagizwa kuwasimamisha kazi watumishi watatu wa halmashauri hiyo.

Tarime.  Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima, amemuagiza katibu tawala mkoa wa Mara kuwasimamisha kazi watumishi watatu wa halmashauri hiyo.

Malima ametoa agizo hilo leo Aprili 9, 2019 baada ya kupokea taarifa kutoka kwa kamati maalumu iliyoundwa kuchunguza matumizi ya zaidi ya Sh9.4 bilioni zilizotolewa na mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara kama ushuru wa huduma.

Watumishi alioagiza kusimamishwa ni mkuu wa idara ya mifugo ambaye aliwahi kukaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Dk  Peter Nyanja; ofisa mipango, Samuel Magige; na mweka hazina wa halmashauri hiyo.

Katika hatua nyingine, Malima ameitaka Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) kumchunguza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tarime vijijini, Apoo Tindwa, kufuatia tuhuma mbalimbali zilizotolewa dhidi yake na kamati hiyo.

Amesema miongoni mwa mambo yaliyobainika kwenye uchunguzi wa kamati hiyo iliyofanya kazi kwa mwezi mmoja ni matumizi yasiyothibitishwa ya zaidi ya Sh1.035 bilioni, baada ya kukosekana kwa nyaraka zinazohalalisha matumizi hayo.

"Uchunguzi umebaini kuwa zaidi ya Sh630 milioni ambazo zilipaswa kuwekwa kwenye mfuko wa wanawake, vijana na walemavu hazikupelekwa kuanzia Julai 2015 hadi Desemba 2018," amesema Malima.

Pia,  ameagiza kutafutwa kwa aliyewahi kuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Athuman Akalama, ili ahojiwe na Takukuru kuhusu tuhuma zilizobainika wakati wa uchunguzi kwani zilitokea akiwa mtumishi wa nafasi hiyo.