Takukuru yaomba kumhoji mshtakiwa mwenye makosa 100

Muktasari:

  • Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa (Takukuru) imeiomba mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu kumhoji mshtakiwa wa tano, Xavery Kayombo anayekabiliwa na mashtaka 100 yakiwemo 24 ya utakatishaji fedha Sh1.17 bilioni

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa (Takukuru) imeiomba mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu kumhoji mshtakiwa wa tano, Xavery Kayombo anayekabiliwa na mashtaka 100 yakiwemo 24 ya utakatishaji fedha Sh1.17 bilioni.

Wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya vitambulisho (Nida), Dickson Maimu, meneja biashara wa Nida, Aveln Momburi, mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, ofisa usafirishaji, George Ntalima na mkurugenzi wa sheria, Sabina Raymond.

Leo Jumanne Februari 12, 2019 wakili wa Takukuru, Leonard Swai amedai mbele ya hakimu mkazi mkuu, Salumu Ally kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutolewa maelezo ya mashahidi.

Amedai Kayombo anatakiwa akahojiwe  na kubainisha kuwa  taarifa za watuhumiwa zimeandaliwa kwa ajili ya kwenda Mahakama Kuu lakini hadi sasa hawajapata rekodi na hawajui wamekwamia wapi.

Baada ya maelezo hayo wakili wa utetezi, Benjamin Mwaleagamba amedai  rekodi zinaonyesha upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wameshawahoji watuhumiwa.

Amedai mara ya mwisho upande wa mashtaka waliwaeleza wameshawasilisha taarifa za mashahidi na waliwatajia hivyo wanapata ukakasi kwani hata mpangilio wa kesi haujawa tayari.

"Tumeambiwa taarifa zipo tayari sababu za kimsingi hazijatolewa za kumtaka mtuhumiwa ahojiwe, ombi hili halina nia nyingine bali wanataka kuchelewesha usikilizwaji wa shauri hili hivyo tunaomba ombi hili likataliwe,” amesema.

Hakimu Ally alikubali ombi la kuhojiwa kwa mshitakiwa huyo na kutaka leo arudishwe rumande kabla muda wa washitakiwa kurudi gerezani haujaisha.

“Wakati mwingine upande wa mashtaka mnapaswa kusema ukweli na wasiseme jambo lolote kwa ajili ya kumfurahisha mtu," alisema Hakimu Ally.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 19, 2019 kwa ajili ya maelezo ya mashahidi.

Katika kesi ya msingi kati ya mashtaka 100, mashtaka 24 ni ya kutakatisha fedha, 23 ya kughushi, 43 ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, mashtaka matano ni ya kuisababishia hasara mamlaka hiyo.