Takukuru yashtukia mbinu mpya ya kuiba dhahabu, sasa vilainishi vyatumika

Muktasari:

Udanganyifu huo kupitia vilainishi kutoka nje, umegundulika katika mgodi wa Stamigold Wilayani Biharamulo


Bukoba. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kagera, imebaini mbinu mpya ya uibaji wa madini ya dhahabu kupitia vilainishi vinavyowezesha kiasi kikubwa kubaki kwenye makinikia baada ya uchenjuaji.

Akitoa taarifa ya utendaji wa Taasisi hiyo kwa miezi tisa leo Juni 7,2019, Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoa wa Kagera, John Joseph amesema udanganyifu huo kupitia vilainishi kutoka nje, umegundulika katika mgodi wa Stamigold Wilayani Biharamulo.

Amesema kupitia vilainishi hivyo, kiasi kikubwa hubaki kwenye mchanga baada ya uchenjuaji na mabaki huchukuliwa kwenda kufanyiwa uchenjuaji mpya na kupata kiasi kikubwa cha madini hayo.

“Tumegundua udanganyifu kwa wanaopeleka vilainishi kwa ajili ya kuchenjua dhahabu kwenye mgodi wa Tulawaka (Stamigold), badala ya kupata gramu 100,  unapata kumi na wanachukua mabaki kwenda kufanya uchenjuaji upya,” amesema Joseph.

Hata hivyo, hakutaja kiasi cha dhahabu na thamani yake vinavyokadiriwa kuibiwa kupitia mbinu hiyo.

Bali almesema mbinu hiyo imekuwa ikitumika kwa takribani miaka miwili sasa na kubainisha kuwa utaratibu za kisheria umeanza kuchukuliwa.

Kuhusu miradi ya barabara iliyotelekezwa na makandarasi wa Manispaa ya Bukoba licha ya kulipwa sehemu ya fedha, Mkuu huyo wa Takukuru Joseph amesema uchunguzi upo katika hatua za mwisho na taarifa itatolewa.

Ametaja baadhi ya maeneo yenye kero za vitendo vya rushwa kuwa ni pamoja na ardhi, polisi kubambikiza kesi na Taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa Sh7.8 bilioni ambazo zingepotea kupitia miradi mbalimbali.