Takwimu za ukataji miti zinatisha A. Mashariki

Muktasari:

Katika mfululizo wa makala zetu za matumizi ya nishati na mazingira, leo tunaendelea kuangalia jinsi mahitaji ya mkaa yanavyozidi kukua kadri idadi ya watu inavyoongezeka.

Matumizi ya mkaa majumbani na viwandani yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kadri idadi ya watu inavyoongezeka, hali inayofanya athari yake katika mazingira kuonekana dhahiri.

Uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa unaotokana na matumizi ya mkaa, ambao unatumiwa na karibu kila kaya unatokana na nishati nyingine za matumizi ya nyumbani kuwa ghali.

Pamoja na uvumbuzi wa nishati mbadala kwa matumizi ya nyumbani, bado matumizi ya mkaa yanatarajiwa kuendelea kuongezeka katika miongo ijayo, hasa barani Afrika kutokana na ongezeko la watu, ukuaji wa miji na bei za nishati mbadala kuwa juu. Pia uwezo duni wa kiuchumi wa wananchi katika mataifa yanayoendelea.

Hadi kufikia 2015, uzalishaji wa mkaa duniani ulikadiriwa kuwa tani milioni 52 kwa mwaka, na kati ya hizo asilimia huzalishwa barani Afrika wakati Amerika ni asilimia 19.6. Kati ya tani milioni 32.4 zinazozalishwa Afrika, asilimia 42 zinazalishwa katika ukanda wa Afrika Mashariki unaohusisha nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi. Afrika Magharibi inazalisha asilimia 32, Afrika ya Kati (12.2), Kaskazini (9.8) na Kusini mwa Afrika ni asilimia 3.4.

Tanzania yaongoza EAC

Tanzania ndio inayoongoza ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuzalisha kiwango kikubwa cha mkaa na inashika nafasi ya saba katika nchi kumi zinazoongoza kwa uzalishaji wa mkaa kwa wingi duniani, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2015.

Nchi nyingine kwenye orodha hiyo ni pamoja na Brazil, Nigeria, Ethiopia, India, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Ghana, China, Madagascar na Thailand.

Tanzania inapoteza takriban eka 150,433 za misitu kila mwaka inayokatwa kwa ajili ya kuzalisha mkaa. Inakadiriwa kuwa kutokana na ongezeko la idadi ya watu, ifikapo mwaka 2030 eka milioni 2.8 za misitu zitakuwa zimepotea.

Zaidi ya asilimia 71.2 ya wananchi Tanzania Bara wanategemea kuni kama nishati ya kupikia, huku asilimia 37.0 wakitumia mkaa na asilimia 5.0 mafuta ya taa.

Jumla ya Dola 350 milioni za Marekani ya mapato yatokanayo na mauzo ya mkaa kila mwaka zinakadiriwa kutoka Dar es Salaam pekee, wakati mapato ya kila mwaka yanayotokana na kahawa na chai yanakadiriwa kuwa Dola 60 milioni za Marekani.

Mkaa wachangia Sh3.5 bil Kenya

Hali ni tofauti nchini Kenya ambako mkaa unakadiriwa huchangia takribani Dola 1.6 bilioni za Marekani kila mwaka kwenye uchumi.

Mahitaji ya mbao nchini humo ni takriban mita milioni 41.7 za ujazo wakati mita milioni 18.7 za ujazo hutumika kama kuni huku mita milioni 16.3 za ujazo hutumika kutengeneza mkaa. Hata hivyo, kinachoweza kuvunwa ni mita milioni 31 za ujazo.

Takriban tani 1.6 milioni za mkaa zinazalishwa kila mwaka, kiasi hiki ni sawa na mauzo ya Dola 400 milioni. Mpaka kufikia mwaka 2013, wazalishaji wa mkaa waliongezeka kwa asilimia 25 hadi kufikia watu 253,808 ambao walikuwa wakizalisha tani 2.5 milioni.

Kwa mujibu wa tafiti zilizofanya na Taasisi ya Huduma za Misitu Kenya (KFS), thamani ya mauzo ya mkaa kwa mwaka 2013 ilifikia Dola 1.6 milioni za Marekani, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 400.

Kwa mwaka 2013, wastani wa mauzo kwa kuangalia mtu mmoja anayezalisha magunia 30 ulikuwa Dola 95 kwa mwezi kulinganisha na gharama ya usafirishaji ambazo zilifikia Dola 2,150.

Uganda waiamini misitu ya asili

Nchini Uganda, wazalishaji wanaiamini zaidi misitu ya asili kuwa ndio inayotoa mkaa bora. Tani milioni 16 za miti hutumika kila mwaka kuzalisha tani milioni 1.8 za mkaa.

Zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wa Uganda wanategemea nishati ya asili itokanayo na mabaki ya mimea na wanyama kwa matumizi tofauti. Mkaa hupendelewa zaidi kwa sababu ni nafuu na rahisi kuusafirisha. Utafiti uliofanyika mwaka 2015 unaonyesha kuwa uoto wa asili ulipungua kutoka asilimia 45 mwaka 1990 mpaka kufikia asilia 11.7 mwaka 2013 kutokana na ukuaji wa miji na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya nusu ya misitu imepotea katika kipindi cha miaka 30 na bado mahitaji yanaongezeka mwaka hadi mwaka.

Uganda inazalisha ajira zaidi ya 20,000 kutokana na mkaa na uzalishaji wa mkaa na kuni huchangia kati ya Dola 26.8 milioni na 48 milioni katika Pato la taifa hilo kwa mujibu wa utafiti huo.

Rwanda yadhibiti mkaa

Wakati Tanzania, Kenya na Uganda zikihaha kukabiliana na ongezeko la matumizi ya mkaa, Rwanda ndio nchi pekee iliyofanikiwa kudhibiti maliasili hiyo na pia kufanikiwa kuongeza uoto wa misitu kwa eka 117,000 kati ya mwaka 1990 na 2010.

Benki ya Dunia (WB) imeeleza kuwa misitu ilichukuwa takriban asilimia 12.9 ya ardhi nchini humo 1990 na mpaka kufikia 2015, eneo la misitu lilikuwa limeongezeka hadi kufikia asilimia 19.5.

Mwaka 2003, mauzo ya mkaa sokoni yaliongezeka hadi kufikia Dola 30 milioni za Marekani (kwa mujibu wa ripoti ya benki hiyo ya 2006). Kutokana na ukuaji wa miji na kupungua kwa misitu, kuna haja ya kuundwa kwa sera ili kukabiliana na changamoto kwenye sekta hiyo.

Katika miaka ijayo Rwanda inatarajia kutumia asilimia 25 ya mkaa kwa mji wa Kigali. Miji mingine itatumia asilimia 40 na iliyosalia vijijini, lakini matumizi hayo yanatarajiwa kushuka kutokana na ongezeko la matumizi ya nishati mbadala.

Ukataji miti waisumbua Burundi

Tatizo la ukataji miti linaisumbua Burundi ambako matumizi ya kuni na mkaa ni asilimia 90. Tatizo la ukataji miti limeifanya ardhi ya Burundi kuwa na asilimia tisa pekee ya misitu ambacho ni kiwango kikubwa duniani cha matumizi mabaya ya rasilimali hiyo.

Kati ya mwaka 1990 na 2010 Burundi imepoteza wastani wa eka 5,850 sawa na asilimia 2.02 za misitu kila mwaka. Kwa ujumla katika kipindi hicho Burundi ilipoteza asilimia 40.5 ya misitu sawa na eka 117,000.

Mpaka kufikia 2010 asilia 6.7 sawa na ekari 172,000 ya ardhi ya Burundi ilikuwa na misitu hii imeifanya kuwa moja kati ya nchi zenye upungufu mkubwa wa nishati zitokanazo na misitu.

Misitu hatarini Sudan Kusini

Nchini Sudan Kusini, utafiti wa mwaka 2015 uliofanywa na FAOSTAT unaonyesha mkaa uliozalishwa ulikuwa tani 272,000 ambao ni sawa na asilimia 0.5 ya dunia ya uzalishaji duniani.

Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori (WCS) imeripoti kuongezeka kwa kasi ya vitendo vya ukataji miti, hali inayotishia ukuaji na uwepo wa misitu.

Utafiti mwingine uliofanywa na Umoja wa Mataifa unaonyesha kuwa katika mji mkuu wa Juba, asilimia 80 ya makazi hutumia mkaa. Pia asilimia 74 na 40 ya taasisi hutumia nishati hiyo.

Vilevile, asilimia 15 ya familia hutumia mkaa, huku asilima nane za biashara na asilimia 40 za taasisi zinategemea kuni kama nishati. Makadirio yanaonyesha kuwa jumla miti milioni tano hukatwa kila mwaka ili kuweza kufikia mahitaji mkaa ya mji wa Juba.

Ripoti ya hali ya mazingira ya mwaka 2018 inaonyesha kuwa asilimia 80 ya miti inayokatwa nchini humo hutumika kuzalisha mkaa na kuni ukataji miti Sudan Kusini unakadiriwa kuwa kati ya asilimia 1.5 mpaka 2.