Tamisemi yajitetea kutohamia kwenye pagale

Muktasari:

  • Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwita Waitara amesema hawajahamia rasmi Mtumba kutokana na miundombinu kutokamilika

Dodoma. Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), hawajahamia rasmi katika jengo lao katika mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma lakini wanaendelea kutoa huduma huko.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri Tamisemi,  Mwita Waitara akizungumza na Mwananchi Digital katika viwanja vya Bunge jana Jumatatu Mei 6, 2019 na kwamba watahamia rasmi katikati ya mwezi ujao.

Waitara alitoa sababu za kutohamia rasmi katika eneo hilo ni miundombinu ya jengo haijawa rafiki hata kwa kupeleka vifaa kama kompyuta na nyaraka mbalimbali.

Aprili 17, 2019 Rais John Magufuli alizindua rasmi ofisi za wizara zote katika mji wa Serikali huku akiagiza mawaziri kuhamia hata kama ni kwenye miembe.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa utetezi kwa Wizara ya Tamisemi na ofisi ya Waziri Mkuu Sera kwamba ujenzi wake ulikuwa nyuma ukilinganisha na majengo mengine kutokana na sababu mbalimbali ikwamo fedha zake kuchelewa.

Wizara zote zilishahamia katika ofisi zao na Tamisemi walipeleka meza mbili na viti sita wakiweka katika vyumba viwili vya mabati ambavyo hutumika kuhifadhia vifaa vya ujenzi.

"Huduma tunatoa kama kawaida lakini mazingira hayaturuhusu kupeleka hata kompyuta, ujenzi umepamba moto na tuko katika hatua nzuri sana, mwezi ujao tutahamia rasmi kwa kila kitu," amesema Waitara.

Naibu Waziri amesema yeye pamoja na waziri mara nyingi wanakuwa huko hata katibu mkuu, lakini kama kuna kazi ya kufanya hata kusaini mafaili lazima warudi mjini.

Waitara amesema vumbi linalotimka katika eneo la ujenzi ni moja ya sababu ya kutokupeleka hata kompyuta moja huko.