Tamwa waomba jamii kushiriki vita ya ukatili kwa wanawake

Saturday May 25 2019

Mkurugenzi wa Tamwa  visiwani Zanzibar, Mzuri

Mkurugenzi wa Tamwa  visiwani Zanzibar, Mzuri Issa. 

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) upande wa Zanzibar kimeiomba jamii kutoa ushirikiano  kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikimo kubakwa hadi kufa.

Kimesema lengo ni kuhakikisha kuwa wahalifu na mashahidi wanafika katika vyombo vya sheria ili haki iweze kupatikana.

Hayo yameelezwa katika taarifa ya chama hicho iliyotolewa leo Jumamosi Mei 25, 2019 na mkurugenzi wa Tamwa  visiwani Zanzibar, Mzuri Issa.

Kupitia taarifa hiyo anaeleza kuwa zaidi ya kesi 17 zimeripotiwa ndani ya miaka mitatu  kuanzia 2016 hadi 2019, zikihusisha wasichana na wanawake kufanyiwa ukatili hadi kufa.

“Lakini hadi sasa hukumu za kesi hizo hazijaweza kutoka kutokana na kile kinachoelezwa kutokujulikana kwa wahalifu.”

“Ni vyema vyombo vya sheria ikiwemo mahakama kuelewa kuwa anayefanyiwa matendo haya huumia kisaikolojia hivyo busara inahitajika ili haki iweze kutolewa pande zote,” ameeleza  Issa katika sehemu ya taarifa yake.

Advertisement

Inafafanua, “Mfano Julai 18,  2018 Wasila Mussa (21) alibakwa na kundi kisha kuuawa huko Tunguu Kichangani Mkoa wa Kusini Unguja na Januari, 2019 msichana mmoja alitupwa huko Kisauni Mkoa wa Mjini Magharibi tayari akiwa amefariki na uchunguzi  ulibaini kuwa alibakwa na watu wengi kabla ya kuuawa.
Hata hivyo, amesema Zanzibar imejitahidi kutunga sheria kali dhidi ya watendaji wa matendo hayo maovu ambayo jamii kwa ujumla inahitaji kusimama imara kuyafichua na kuyakomesha.

Sheria hizo ni pamoja na sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 7 ya mwaka 2018 inayotoa hadi kifungo cha maisha kwa wahalifu hao na kwamba kutokana na ukubwa wa kesi za namna hiyo hata dhamana kwa washtakiwa hairuhusiwi.

 

Advertisement