Tamwa yapata bosi mpya

Muktasari:

Tamwa yapata mkurugenzi mpya, aliyemaliza muda wake, Edda Sanga asisitiza waandishi wa habari kujiongeza ili kwenda sawa na kasi ya dunia 

Dar es Salaam. Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimefanya mabadiliko kwa uongozi wake baada ya aliyekuwa mkurugenzi, Edda Sanga kumaliza muda wake.

Katika mabadiliko hayo nafasi hiyo imechukuliwa na mwandishi wa habari Rose Reuben.

Akizungumza baada ya kukabidhi kijiti cha uongozi leo Ijumaa Januari 11, 2019 Sanga amesema anajivunia kuunda kamati katika wilaya kadhaa zinazojikita katika kupambana na ukatili wa kijinsia.

“Nilifarijika mno kufika huko na wazee, viongozi wa vyama husika kuonyesha kuelewa kuhusu mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na kuahidi kushiriki kwenye mapambano hayo,” amesema.

Sanga amesema anajivunia kuiacha Tamwa kwa mtu sahihi ambaye ni mwandishi, mwalimu na msomi anayetarajiwa kupata shahada ya uzamivu hivi karibuni.

Sanga amewasisitiza waandishi wachanga kujiongeza ili kwenda na kasi ya maendeleo ya dunia.

Kwa upande wake, Rose amesema makabidhiano ya majukumu ni jambo linaloheshimisha chama hicho huku akiahidi kulipeleka mbele jahazi la Tamwa.

“Tunafahamu ili nchi iweze kuendelea ni lazima kuwepo na wanawake wenye afya njema ya kisaikolojia pamoja na kimwili na hilo litawezekana endapo watatendewa haki,

“Ukatili wa kijinsia haupendezi, niwasihi wanahabari muendelee kuibua mambo yanayosababisha ukatili wa kijinsia. Tunataka hapa kazi iendane na afya njema na haki,”

Amesisitiza kuwa kufikia Tanzania ya viwanda ni lazima wanawake, vijana na watoto watendewe haki jambo litakalowasababisha kuwa wabunifu.