Tanesco yawatangazia neema wakazi wa Kinondoni

Wednesday August 14 2019

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linawataarifu wananchi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam kubadilisha mita zao kwa kuondoa mita zilizokwisha muda wake na mita mbovu na kufungiwa mita mpya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tanesco leo Jumatano Agosti 14,2019 shughuli hiyo inaendelea na  itafanyika katika mkoa wa kihuduma wa Kinondoni Kaskazini ambayo itahusisha wilaya zake zote za Mikocheni, Mbezi na Tegeta.

Taarifa hiyo imesisitiza huduma hiyo ni bure na wateja wa Tanesco watafungiwa mita nyingine baada ya kuondolewa kwa ile ya zamani.

Tanesco imebainisha wafanyakazi wake watakuwa na magari ya shirika yenye namba za usajili zinazoanzia na SU pamoja na vitambulisho vyao vya  kazi.

“Tunaomba ushirikiano wako wakati wa utekelezaji wa zoezi hili kwa wafanyakazi kutoka Tanesco ili kufanikisha kazi hii muhimu, wafanyakazi watakuwa na magari ya Shirika yanayoanzia na namba SU… pamoja na vitambulisho vyao vya  kazi.”

“Shirika linapenda kukuhakikishia utakapobadilishiwa mita ya zamani wakati huohuo utafungiwa mita mpya na unit ambazo zilizokuwa katika mita ya zamani utarudishiwa kwa utaratibu wa shirika ulioandaliwa ofisini,” inafafanua taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Uhusiano.

Advertisement

Advertisement