Tanesco kutengeneza faida ya Sh9 bilioni

Sunday June 30 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Shinyanga. Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani ameeleza mambo kadhaa yanayochangia mafanikio ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuweza kujiendesha lenyewe bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga, Juzi Jumamosi Juni 29, 2019, muda mfupi kabla ya kutembelea Kijiji cha Mwakitolyo kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, Waziri Kalemani alisema sababu kubwa ya Shirika kuimarika ni hatua iliyofanywa na Serikali, kuondoa miradi iliyokuwa inazalisha umeme wa mafuta mazito, ambayo uendeshaji wake ulikuwa na gharama kubwa.

Alisema sababu nyingine ni zuio lililotolewa na Serikali kwa Tanesco kuhusu kuagiza vifaa nje ya nchi.

Waziri huyo alisema hiyo pia imechangia hali hiyo na sasa, shirika linahamasisha wazalishaji wa Kitanzania kutengeneza vifaa hivyo ndani ya nchi.

Alisema kabla ya zuio hilo, nguzo zilikuwa zikiagizwa Afrika Kusini, Mita (China), Transfoma ( India) na nyaya zilikuwa zikiagizwa nchi mbalimbali za nje.

“Hii imeokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumiwa na shirika kuagiza vifaa husika nje ya nchi,” alisema Kalemani.

Advertisement

Pia aliupongeza uongozi wa Tanesco na wafanyakazi wake kuwa wamechagiza kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya shirika.

“Shirika letu linaendelea kuimarika sana. Tanesco ya miaka mitano iliyopita ni tofauti na ya sasa. Ya zamani ilikuwa na madeni na hasara, sasa hivi hatuna hasara,” alisema.

Alisema mwaka huu, Tanesco inategemea kutengeneza faida ya Sh9 bilioni tofauti na miaka mitatu iliyopita, ambayo lilipata hasara ya Sh349 milioni.

Akizungumzia ruzuku iliyokuwa ikitolewa kwa shirika hilo awali, Kalemani alisema  lilikuwa  likipatiwa Sh143 bilioni, lakini tangu mwaka juzi, shirika hilo linajiendesha lenyewe pasi kutegemea fedha kutoka serikalini.

Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alisema amekwishatoa maagizo kwa mameneja wote wa Tanesco nchini, kuhakikisha umeme haukatiki bila sababu za msingi katika maeneo yao.

“Hakuna sababu ya kukatikakatika umeme kwa sasa, maana tunayo ziada ya takribani megawati 220 hadi 300 kwa siku,” alisisitiza Waziri.

Waziri Kalemani alikuwa katika ziara ya siku moja mkoani Shinyanga, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.


Advertisement