Tanesco yaitwisha Serikali zigo la deni

Wednesday March 20 2019

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali imeombwa kubeba deni la Sh1.39 trilioni ambalo Shirika la Umeme nchini (Tanesco) linadaiwa na taasisi mbalimbali ikiwamo watoa huduma wake na mabenki.

Katika deni hilo, Sh950 bilioni zinadaiwa na watoa huduma ikiwamo kampuni za IPTL, Songas, Pan African na TPDC, huku Sh442 bilioni zikiwa ni ilizokopa benki kwa matumizi mbalimbali.

Jana wakati kamati ya bunge, uwekezaji mitaji ya umma ilipotembelea mradi wa umeme wa Kinyerezi, mkurugenzi wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka alisema Sh408 bilioni ilikopa benki kwa ajili ya kununulia mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kufua umeme.

Pia alisema Sh34 bilioni zilizokopwa benki ya uwekezaji nchini (TIB) zilikuwa ni kwa ajili ya kulipa fidia ya ujenzi wa laini kutoka Somangafungo hadi Kinyerezi.

Tito alisema madeni hayo ni ya miaka ya nyuma wakati wakifua umeme kwa kutumia vyanzo ghali ambavyo vilikuwa vinafanya gharama ya kuzalisha umeme kuwa kubwa ikiwamo kukodisha kampuni kama IPTL na matumizi ya mafuta mazito na kwamba wamekuwa wakiendelea kuyalipa lakini yanaongezeka kutokana na riba.

“Tunaiomba Serikali kupitia Hazina kuyalipa madeni hayo ili kuipunguzia mzigo Tanesco,” alisema.

Advertisement

Dk Mwinuka alisema kwamba shirika hilo halifanyi vizuri kunatokana na kuwa zamani lilikuwa likitumia mafuta mazito ambayo bei yake ni ya juu lakini kwa sasa kwenye gesi kuna nafuu na inaweza kuwa chini zaidi kama gharama za bomba zitachukuliwa na Serikali.

Alisema Tanesco ilikuwa ikitengeneza hasara, ambapo mwaka 2016/17 ilipata hasara ya Sh 265 bilioni, 2017/18 hasara Sh 124 bilioni lakini mwaka huu wanatarajia kutengeneza faida ya Sh9 bilioni.

Meneja wa mradi wa umeme wa Kinyerezi, Ernest Nzemya alisema mradi huo wa megawati 150 ulianza Agosti 2013 na Oktoba 17, 2015 ulizinduliwa rasmi na gharama yake ni dola 183 milioni za Marekani sawa na Sh402.6 bilioni na kwamba utakapokamilika utazalisha megawati 575 za umeme.

Alisema mradi huo una mashine nne zinazotumia mafuta ya ndege au gesi na kutoa megawati 150. “Tunatumia gesi kiasi cha mmbtu 33,000 kwa siku ambayo kwa bei tunayonunua TPDC inagharimu Sh400 milioni lakini katika kiasi hicho cha gesi tunazalisha uniti 3.5 milioni kwa siku ambayo ukipiga ‘revenue’ ni kama Sh800 milioni kabla hujaweka vitu vingine ikiwamo matengenezo.

Advertisement