Tanesco yatimua mameneja saba

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba akizungumza na waandishi wa habari.

Muktasari:

Juzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kagera, miongoni mwa viongozi hao, Isaack Tibita na Olver Mushumbuzi waliokuwa mameneja kwa nyakati tofauti wilayani Karagwe walipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kutenda makosa 16 wakishirikiana na raia wa China.

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limewaachisha kazi wafanyakazi wake saba wa kada ya uhasibu, umeneja na uhandisi kwa tuhuma za wizi na ubadhirifu.

Juzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kagera, miongoni mwa viongozi hao, Isaack Tibita na Olver Mushumbuzi waliokuwa mameneja kwa nyakati tofauti wilayani Karagwe walipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kutenda makosa 16 wakishirikiana na raia wa China.

Viongozi hao wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema jana kuwa watumishi hao waandamizi wamefukuzwa kazi na shirika hilo.

Mbali na Kagera watumishi wengine wanatoka mikoa ya Kinondoni Kaskazini, Ilala na Katavi.

Alisema mara kwa mara wamekuwa wakipata kero kutoka kwa wateja wao kuhusu kudaiwa rushwa kabla ya kupewa huduma.

“Mfanyakazi yeyote wa Tanesco atakayebainika analaghai wateja, anadai rushwa au anatoa lugha chafu atawajibishwa mara moja na ataachishwa kazi,” alisisitiza Mhandisi Mramba.

Alisema Tanesco imedhamiria kupambana na hali hiyo ndiyo maana ipo katika maandalizi ya mwisho ya kuandaa namba maalumu za simu kwa wateja wao.

Alisema namba hizo zitatumika kutoa taarifa ya vitendo vinavyofanywa na watendaji wa shirika hilo dhidi yao ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Pia, Mkurugenzi huyo amewapa siku saba wateja wa shirika hilo ambao mita zao zimechezewa na kutumia umeme kinyume cha sheria na kujisalimisha kwa mameneja husika wa mikoa kabla hawajachukuliwa hatua.