Tanesco yatoa sababu za kukatika kwa umeme

Wednesday January 9 2019Ofisa Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji

Ofisa Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar er Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limetangaza kuanzia leo Januari 9 hadi Februari 13, baadhi ya maeneo ya mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar yatakuwa yakikosa umeme kutokana na ukarabati wa mashine katika kituo cha kufua umeme kwa gesi cha Ubungo II.

Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam leo Januari 9, 2019, Ofisa Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji alisema ukatikaji huo wa umeme hautakuwa ukichukua muda mrefu kama baadhi ya wateja wao wanavyodhania.

“Baadhi ya maeneo yatakuwa yakikosa umeme kwa takribani saa moja au mbili kulingana na matengenezo ya siku husika, mikoa hiyo haiwezi kuingia gizani,” alisema Leila.

Hata hivyo, alisema ukarabati huo ni wa kawaida kufanyika kulingana na maelekezo ya matumizi ya mitambo hiyo ya kufua umume kwa gesi.

“Hii mitambo inatakiwa itembee kwa saa 40,000 kulingana na maelekezo, kisha inafanyiwa ukarabati, ni kama mtu anavyopeleka gari yake gereji ikiwa imetembea kilomita kadhaa baada ya service, na hii mitambo ya kufua umeme kwa gesi inatakiwa ifanyike hivyo. Ikilazimishwa kufanya kazi zaidi ya saa hizo bila kufanyiwa ukarabati, inaweza ikaharibika,” alisema ofisa huyo.

Akizungumzia muda wa matengenezo na kama ukarabati huo utakuwa na athari kwa watu waishio au kupita jirani na mitambo hiyo, alisema hayana madhara yoyote kwa binadamu.

Advertisement