Serikali ya Tanzania kugharamia matibabu ya waliojeruhiwa Msumbiji

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa akikabidhi rambirambi kwa mmoja wa ndugu waliopoteza maisha baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika kijjji cha Mtole nchini Msumbiji. Picha na Haika Kimaro

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imeahidi kugharamia matibabu ya watu waliojeruhiwa na watu wasiojulikana katika kijiji cha Mtole nchini Msumbiji na kukabIdhi  rambirambi kwa wafiwa.

Mtwara. Serikali ya Tanzania imesema itagharamia matibabu ya wananchi waliojeruhiwa katika kijiji cha Mtole nchini Msumbiji mpakani mwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia kwa amani na utulivu.

Hatua hiyo inakuja baada ya Watanzania kumi kuuliwa na watu wasiojulikana katika kijiji cha Mtole nchini Msumbiji kwa kupigwa risasi na wahalifu hao Juni 26, 2019 na baadhi kujeruhiwa ambao walikuwa wakipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Ligula mkoani Mtwara.

Ahadi hiyo imetolewa leo Alhamisi Julai 18,2019 na mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa katika kijiji cha Kitaya kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji alipokuwa akikabidhi rambirambi kwa wafiwa.

Aidha amesema kuhusu mwanamke mmoja na mtoto aliyetekwa na wahalifu hao wamelipa jukumu jeshi la polisi katika maongezi na jeshi la Msumbiji kuhakikisha wanapatikana.

“Kuhusu mama aliyepotea tumelipa jukumu jeshi la polisi katika maongezi na wenzao wa Msumbiji kuhakikisha tunampata na tungependa kumpata akiwa hai, vyombo vyetu vinafanya kazi nzuri tuendelee kuviamini na sisi wenyewe tukijenga mshikamano na tunatoa taarifa Tanzania tutaendelea kuwa kisiwa cha amani,” amesema Byakanwa

“Na watu ambao hawana amani kwenye nchi zao wataendelea kuikimbilia Tanzania ndio maana wale wa Msumbiji walipoingia hapa tumewatibu pamoja na wale Watanzania na gharama zao zitalipwa na Serikali, kwa hiyo tuna jukumu la kuendelea kuitunza tunu yetu hii ya amani na utulivu,” amesema

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda amesema katika majeruhi waliokuwa nane mmoja amehamishiwa kitengo cha mifupa MOI, Dar es Salaam na wengine sita wameruhusiwa kutoka hospitali.

“Majeruhi walikuwa nane miongoni mwao wakiwa wa Msumbiji, majeruhi sita wameruhusiwa lakini mmoja  kutokana na tatizo lake kuonekana kubwa amepata rufaa kupelekwa kitengo cha mifupa Moi Muhimbili na mmoja naambiwa amefariki na kufanya idadi ya Watanzania waliokufa kuwa 11,”amesema Mmanda