Tanzania kuijibu Marekani, Uingereza

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema inalifanyia kazi tamko la pamoja la ubalozi wa Marekani na Uingereza linaloelezea wasiwasi wa kuzorota kwa haki za raia nchini.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inalifanyia kazi tamko la pamoja la ubalozi wa Marekani na Uingereza linaloelezea wasiwasi wa kuzorota kwa haki za raia nchini.

Katika tamko hilo lililotoka leo Ijumaa Agosti 9, 2019 mabalozi hao wanaitaka Serikali kutoa hakikisho la mchakato wa kutenda haki kwa raia wake.

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Agustine Mahiga akizungumza na Mwananchi leo kuhusu tamko hilo amesema wameliona na wanalifanyia kazi.

Mwanadiplomasia huyo amesema wizara yake   pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) watakutana kujadili tamko hilo na baada ya hapo Serikali itatoa msimamo.

“Baada ya  kukaa kwa pamoja tutatoa taarifa ya Serikali kuhusu tamko hilo la pamoja,” amesema  Balozi Mahiga aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Amesema anafahamu tamko hilo linatokana na tukio la hivi karibuni ambalo hakulitaja.

Katika tamko hilo, mabalozi wanaeleza kusikitishwa na matukio ya mara kwa mara ya watu kuwekwa  kizuizini kwa muda bila kupelekwa mahakamani na kubadilishiwa mashtaka na mamlaka za kisheria, wakitolea mfano mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera ambaye hivi sasa anashikiliwa na vyombo vya dola.

“Tuna wasiwasi hasa kwa tukio la karibuni jinsi ambavyo halikushughulikiwa kwa haki, la kukamatwa na kuwekwa kizuizini la Kabendera ukizingatiwa ukweli kwamba alinyimwa haki ya kuwa na mwanasheria kwenye hatua za awali za kutiwa kizuizini ambapo ni kinyume cha sheria ya makosa ya jinai,” linaeleza tamko hilo.

Tamko hilo lilitoa wito kwa Serikali hapa kutoa hakikisho cha mchakato haki hizo kama ambavyo inazitambua kuwa ni haki za msingi kwakuwa imeridhia mikataba mbalimbali ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (UN), miongoni mwake likiwemo azimio la kimataifa la haki za kisiasa.