VIDEO: Tanzania kuiuzia Kenya tani milioni moja za unga na mahindi

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe katika kikao cha majadiliano kati ya viongozi wa idara, taasisi zilizo chini ya wizara yake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Kenya, Profesa Hamadi Boga (kulia) na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu (kushoto), kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara hiyo jijini Dar es Salaam leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

 

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imekubali kuiuzia Kenya tani milioni moja za mahindi na unga ndani ya mwaka mmoja ili kuiwezesha nchi hiyo  kukabiliana na uhaba wa chakula.

Dar es Salaam. Tanzania itaiuzia Kenya tani milioni moja za unga na mahindi katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa ili kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na uhaba wa chakula uliosababishwa na mvua hafifu msimu iliopita.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofanyika kati ya Rais John Magufuli na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta walipokutana Chato, Geita Julai 2019.

Leo Alhamisi Julai 25, 2019 naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameongoza majadiliano kati ya idara zilizo chini ya wizara yake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Kenya, Profesa Hamadi Boga na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu.

Bashe amesema taasisi za Serikali zianze kufikiria kibiashara ili kunufaika na fursa ya soko la Kenya na kuwawezesha wafanyabiashara kwenda kuuza unga au nafasi nchini Kenya.

“Wenzetu wanasema asilimia 50 ya pato la Mkenya linatumika kwenye chakula, tunaomba hali ibaki hivyo ili tuitumie hii fursa,” amesema Bashe na kuwafanya washiriki wengine wa kikao hicho kucheka.

Bashe ambaye aliapishwa Jumatatu Julai 22, 2019 kuwa naibu waziri wa wizara hiyo amezitaka taasisi zote za Tanzania na Kenya zinazohusika katika ununuzi n a usafirishaji wa unga na mahindi, kukutane na kupanga mikakati ya kufanikisha suala hilo.

Profesa Boga amesema upungufu wa chakula uliopo Kenya umesababishwa na uhaba wa mvua katika msimu uliopita, jambo ambalo limeathiri kilimo kwenye maeneo yanayozalisha chakula kwa wingi nchini humo.

“Kutokana na changamoto hiyo, tuna upungufu wa tani milioni moja kwa mwaka. Tukipata kiasi hicho kitatutosha kwa mwaka mzima,” amesema Profesa Boga ambaye aliambatana na ujumbe wa Rais Kenyatta ulioleta fedha na dhahabu za Tanzania ziliyokamatwa Kenya.

Taasisi za serikali zilizohudhuria kikao hicho ni pamoja na Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Idara ya Usalama wa Chakula (DNFS) na Idara ya Maendeleo ya Mazao (DCD) kutoka Wizara ya Kilimo.