Tanzania kuwa na uchumi wa kati mwaka 2020

Dar es Salaam. Kutokana na ukuaji mzuri wa uchumi kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, Benki ya Dunia (WB) imesema hadi mwaka 2020 Tanzania itakuwa na uchumi wa kati.

Hilo limebainishwa leo Alhamisi Julai 18, 2019 na mkurugenzi mkazi wa benki hiyo nchini Tanzania, Bella Bird katika uzinduzi wa ripoti ya 12 ya hali ya uchumi Tanzania iliyoangazia umuhimu wa rasilimali watu katika kukuza utajiri.

Bella amesema muda wowote kuanzia sasa Tanzania itaingia kwenye orodha ya nchi za chini zenye uchumi wa kati (LMIC).

“Ili kuwa LMIC kila pato la mwananchi linapaswa kuwa Dola 1,025 za Marekani, mpaka sasa pato la kila Mtanzania ni Dola 1,020 hivyo muda wowote kuanzia sasa mpaka mwakani Tanzania itaingia kwenye orodha hiyo,” amesema Bella.

Kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, ukuaji wa uchumi ulikuwa wastani wa asilimia 7.0 hali iliyosaidia kuimarisha uchumi nchini.

Kutokana na mwenendo huo mzuri, WB imesema wastani wa pato la kila Mtanzania limeongezeka na dalili zinaonyesha kati ya mwaka 2019 na 2020 itakidhi sifa za kuwa na uchumi wa kati.