Tanzania yaahidi ushirikiano kwa wafanyabiashara wa China

Tuesday February 12 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali imeahidi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji kutoka Hong Kong, China ambao wameonyesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya mazao ya kilimo, dawa na vifaa tiba na sekta ya utalii.

Leo Jumanne  Februari 12, 2019 Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji,  Angellah Kairuki amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka jimbo hilo la kibiashara lililopo Kusini mwa China.

"Tarehe 10 mwezi huu tulipata ujumbe wa wafanyabiashara saba kutoka Hong Kong wamekuja kutafuta fursa za uwekezaji zilizopo nchini, tangu wamefika wametembelea taasisi zetu mbalimbali ikiwemo MSD na EPZA, Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano hata baada ya kufanya maamuzi ya kuwekeza," amesema Kairuki.

Amesema endapo uwekezaji huu utafanyika, Tanzania itanufaika na ajira za wananchi zitakazotolewa, kupata fedha za kigeni kutokana na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi lakini pia kukuza pato la Taifa na kuongeza idadi ya watalii.

Mmoja wa wajumbe hao, Jessica So amesema amefurahishwa na taarifa kuhusu fursa mbalimbali na kuahidi kuwa baada ya kurudi nyumbani anaamini wafanyabiashara wengi watakuja kuwekeza katika viwanda vya mazao ya kilimo, dawa na vifaa tiba na utalii.

Advertisement