Tanzania yang’ara vita dhidi ya rushwa

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema nchi za Bara la Afrika zimeitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa.

Majaliwa alisema hayo akitoa muhtasari wa yaliyojiri kwenye mkutano wa 32 wa wakuu wa nchi za Afrika (AU) unaofanyika Addis Ababa, Ethiopa.

Waziri Mkuu ambaye alimwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano huo alisema licha ya mambo mengine, Serikali barani Afrika zimesisitizwa kupambana na wala rushwa huku Tanzania ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa.

Mbali na kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa, Majaliwa alisema ripoti ya kamati maalumu iliyoundwa kuhusu masuala ya afya inaonyesha Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri.

Alisema Tanzania imefanya vizuri katika kusimamia na kudhibiti malaria, mapambano dhidi ya Ukimwi na utoaji huduma za afya kwa wananchi mpaka vijijini.

“Imetupa faraja kwa sababu ukaguzi uliofanywa na kamati maalumu ya maendeleo ya afya iliyotembelea nchi za Afrika kuona mwenendo wa utoaji huduma imeonyesha tupo kiwango kizuri, ” ilisema sehemu ya taarifa iliyotumwa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu.

Alisema mafanikio hayo yamekuja baada ya Serikali kuongeza bajeti ya afya kutoka Sh37 bilioni hadi Sh269 bilioni.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres alisema licha ya changamoto zote zinazolikabili Afrika, bara hilo limeacha milango yake wazi kwa wakimbizi.