Tanzania yapewa cheti ubora wa huduma za hali ya hewa

Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi

Muktasari:

Akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya hali ya hewa duniani, jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi, Isack Kamwelwe alitoa wito kwa wadau mbalimbali wa huduma za hali ya hewa kushirikiana na Serikali kutekeleza programu ya kitaifa ya huduma za hali ya hewa ambayo ni muongozo muhimu katika utumiaji wa huduma za hali ya hewa nchini.

Dar es Salaam. Tanzania mwaka huu imekuwa miongoni mwa nchi tatu barani Afrika zilizopata cheti cha ubora wa huduma bora za hali ya hewa katika usafiri wa anga (ISO 9001:2015) kinachotolewa na Shirika la Viwango Duniani (ISO)

Hata hivyo, imeelezwa kuwa bado inakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za kununua vifaa vya hali ya hewa vinavyoendana na mabadiliko ya kukua kwa teknolojia katika tasnia ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya hali ya hewa duniani, jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi, Isack Kamwelwe alitoa wito kwa wadau mbalimbali wa huduma za hali ya hewa kushirikiana na Serikali kutekeleza programu ya kitaifa ya huduma za hali ya hewa ambayo ni muongozo muhimu katika utumiaji wa huduma za hali ya hewa nchini.

“Serikali imenunua rada mbili za hali ya hewa ambazo zimewekwa Dar es Salaam na Mwanza na nyingine tatu zinatarajiwa kuwekwa Mtwara, Mbeya na Kigoma ambazo ziko katika hatua ya manunuzi,” alisema.

Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi alisema wanaendelea kupanua mtandao wa vituo vya kupima hali ya hewa kwa kuzingatia makubaliano ya kimataifa (Minamata Convention 2020), ambapo vifaa vyote vinavyotumia zebaki vimewekewa ukomo wa matumizi ifikapo mwaka 2020.

Naye mkugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Hamza Johari alisema lengo ni kuhakikisha usafiri wa anga unakuwa salama pamoja na abiria na mizigo.

Alisema rubani wa ndege kabla ya kuanza safari analazimika kwenda chumba maalumu cha kupata taarifa za hali ya hewa na inapotokea hali ya hewa ni mbaya kwa mujibu wa sheria safari inaahirishwa.