Tanzania yasaidia nchi zilizokumbwa na kimbunga Idai

Wednesday March 20 2019

Askari wa JWTZ wakipakia dawa na chakula kwenye

Askari wa JWTZ wakipakia dawa na chakula kwenye ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana ikiwa ni msaada uliotolewa na Serikali kwa ajili ya wahanga waliokumbwa na kibunga katika nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe. Picha na Anthony Siame 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali imetoa msaada wa chakula na dawa kwa nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe baada ya kukumbwa na kimbunga cha Idai.

Hadi jana jioni, takriban watu 120 walikuwa wanasadikiwa kufariki dunia nchini Msumbiji na Zimbabwe, wakati watu 56 wamefariki kutokana na mafuriko nchini Malawi.

Msaada huo uliotolewa jana jijini Dar es Salaam ni pamoja na dawa za binadamu tani 24, mchele tani 14 na mahindi tani 200.

Zimbabwe na Msumbiji watapata tani saba za mchele na tani nane za dawa kila nchi lakini Malawi itapata tani nane za dawa na tani 200 za mahindi. Thamani ya msaada huo haijatajwa.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Profesa Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu walikabidhi msaada huo kwa mabalozi wa nchi hizo hapa nchini. Misaada hiyo ilisafirishwa kwa ndege ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwenda Zimbabwe na Msumbiji wakati ya Malawi itapelekwa na malori.

Profesa Kabudi alisema misaada hiyo imetolewa na Rais John Magufuli baada ya kupata taarifa za kimbunga kisha kuongea na marais wa nchi hizo kujua hali halisi.

“Sisi tuna wajibu na vifo vya jirani zetu. Shida za majirani zetu ni za kwetu. Leo kwao kesho kwetu,” alisema Profesa Kabudi.

“Huu ni msaada wa Serikali lakini tunatoa wito kwa watu binafsi, mashirika na kampuni nchini kuwachangia hao majirani zetu kupitia ofisi ya Waziri Mkuu.”

Waziri Ummy alisema alipokea maelekezo kutoa kwa Rais na baadaye kuongea na mawaziri wenzake wa nchi hizo.

“Wote waliniambia wanahitaji dawa za kuzuia maambukizi ya bakteria na magonjwa ya tumbo hivyo kwa asilimia kubwa ndizo tulizowapatia,” alisema.

Alisema pia katika msaada huo kuna mashuka, magodoro, blanketi na vitu vingine ambavyo ni muhimu katika shughuli za uokoaji na makazi ya dharura kwa waathirika.

Hata hivyo, Waziri Ummy alisema msaada huo hautaathiri upatikanaji wa dawa nchini na kwamba Serikali iko tayari kutoa msaada wa madaktari watakaoongeza nguvu katika utoaji wa huduma kwa kipindi hiki.

Balozi wa Malawi nchini, Glad Munthali aliona msaada huo kuwa ni maajabu ambayo Serikali ya Tanzania imefanya na hivyo kushukuru.

Balozi wa Zimbabwe, Martin Tavenyika alisema ni upendo mkubwa ulioonyeshwa na Tanzania kwa kuwa wamepewa msaada bila hata kuomba.

Naye Balozi wa Msumbiji, Monica Clemente alisema huo ni msaada mkubwa sana kwa nchi yao kwa kuwa watu wengi wamepoteza maisha.

Watu wapatao 65 wamethibitishwa kufariki nchini Zimbabwe kutokana na kimbunga hicho huku wengine 217 bado hawajaonekana, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Habari ya nchi hiyo.

Nchini Msumbiji, hadi jana jioni watu 62 walifariki, wakati nchini Malawi karibu watu 56 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko huku Serikali ikikadiria watu 83,000 wamekimbia makazi. Umoja wa Mataifa umesema kimbunga kinachokuja kitakuwa na upepo wa kasi ya kilomita 190 kwa saa.

Advertisement