Tathmini usajili wa simu kwa kutumia alama za vidole kufanyika Septemba 2019

Spika wa Bunge, Job Ndugai akiweka alama ya kidole katika kitufe alipokuwa akisajili laini yake ya halotel katika viwanja vya bunge jijini Dodoma leo. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kuandikwa. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye amesema watafanya tathmini ya usajili kwa kutumia  alama za vidole nchini Septemba 30, 2019

Dodoma. Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye, amesema watafanya tathmini ya usajili kwa kutumia  alama za vidole nchini Septemba 30, 2019.

Nditiye ameyasema hayo leo Mei 7, 2019 wakati Spika wa Bunge Job Ndugai alipotembelea zoezi la usajili wa simu kwa kutumia alama za vidole linaloendelea katika viwanja vya Bunge.

Amesema zoezi hilo limeanza rasmi Mei 2019 nchini na lengo Watanzania waweze kuangalia ni nani, ni line gani kwa mtandao gani kwa ajili ya usalama na maendeleo ya nchi.

“Wabunge wengi wamesajili kwa kutumia alama za vidole. Tunamshukuru Mhesimiwa Rais kwa kuongeza muda wa usajili hadi Desemba 31,” amesema.

Amewata Watanzania kusajili simu zao kwa kutumia alama za vidole kwa ajili ya usalama.

“Hii itatusaidia sana kuwapata wote wanaocheza na mitandao na kujaribu kuwaumiza Watanzania wenzetu,” amesema.

Amesema mapokeo ni mazuri na kuwataka watu walio katika maeneo  machache ambayo hawajapata vitambulisho vya taifa, kutumia namba zao za usajili walizozipata kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Spika wa Bunge, Job Ndugai amewahimiza Watanzania kuhakikisha wanajiandikisha Nida ili waweze kushiriki katika kusajili line za simu kwa kutumia alama za vidole.