Televisheni ya Channel 10 sasa ni mali ya CCM

Dar es Salaam. Kituo cha Televisheni cha Channel 10 sasa rasmi kinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya mwenyekiti wake, Rais John Magufuli kuweka bayana mikakati ya kukiboresha ikiwamo kununua vifaa vipya.

Jana, Rais Magufuli alitembelea kituo ambacho kipo chini ya Shirika la African Media Group, ikiwa ni ziara ya kutembelea miradi ya chama hicho tawala ambacho jana kiliadhimisha miaka 42 ya kuanzishwa.

African Media Group inamiliki pia redio ya Magic Fm na Rais Magufuli alisema kituo hicho kwa sasa ni mali ya CCM na akiwa mwenyekiti, ameanza kufanya mabadiliko mbalimbali ili kuhakikisha kinaboreshwa.

“Leo (jana) ni siku muhimu sana kwa chama chetu cha CCM kwa sababu tunatimiza miaka 42 tangu chama chetu kianzishwe kwahiyo nikafikiri niende African Media group niwasalimu kwa sababu ni chombo cha CCM lakini pia nafahamu mmekuwa mkifanya kazi katika vipindi vigumu,” alisema Dk Magufuli.

Alisema pamoja na mabadiliko hayo, hakuna mfanyakazi atakayeondolewa hata kama ni wa chama kingine huku akiwataka kuwa chachu ya maendeleo kwa Taifa.

“Nimeambiwa kuna wafanyakazi 99 sifahamu vyama vyenu lakini ninyi ni Watanzania, uwe Chadema, uwe CUF, uwe huna chama hapa mmekuja kufanya kazi, hongereni sana. Hilo napenda kuwathibitishia tutaendelea kufanya kazi kwa pamoja,” alisema Rais Magufuli.

Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Jafari Haniu alisema changamoto kubwa inayoikabili televisheni hiyo ni madeni ambayo yamedumu kwa miaka zaidi ya 20 tangu kuanzishwa kwake.