Tembo wafungwa mikanda ya GPS

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamis Kigwangallah akishiriki zoezi la kuwafunga mikanda ya GPS Tembo katika eneo la hifadhi ya Jamii ya Makao. Picha Mussa Juma

Muktasari:

  • Tembo wafungwa GPS kwa ajili ya kuwafuatilia na hatimaye kuzuia uvamizi katika mashamba na kupambana na ujangili.

Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangallah amezindua mpango wa kuwafunga tembo vifaa vya mawasiliano ya kijiographia (GPS) ili kuweza kuwafuatilia na kuzuia ujangili na kuvutia watalii zaidi.

Waziri Kigwangallah ambaye jana alishiriki mapokezi ya watalii 343 kutoka China, amesema lengo la Serikali kwa sasa ni kuendelea kuboresha uhifadhi hasa bada ya ongezeko kubwa la tembo na hivyo kuvutia watalii zaidi.

"Vifaa hivi vya GPS vitawawezesha tembo kufuatiliwa mienendo yao na hivyo kuweza kudhibiti matukio ya tembo kuvamia mashamba na masuala ya ujangili kwani pia kutawekwa uzio wa kielekroniki," amesema.

Waziri Dk Kigwangallah aliipongeza taasisi ya Friedkin Conservation Fund (FCF) kwa kufadhili mradi huo na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri) kwa kuendesha zoezi hilo.

Mkurugenzi wa FCF, Nicholas Negri amesema mradi huo utasaidia sana uhifadhi nchini na kuvutia watalii zaidi.

Alisema FCF itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza uhifadhi kwani pia tayari wamefadhili mradi wa kuwafunga vifaa vya mawasiliano faru ili kuwalinda na ujangili.

Mtafiti mkuu wa Tawiri, Dk Edward Kohi amesema mradi huo, unatarajia kugharimu dola 300,000 ambazo ni zaidi ya Sh800 milioni.

Amesema katika eneo la hifadhi ya jamii ya makao na pori la akiba la Maswa, tembo 18 watafungwa vifaa vya GPS.

Mtafiti wa Tawiri, Dk Emmanuel Masenga amesema hadi sasa tembo 95 wamefungwa mikanda ya GPS katika maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini.