Tiger Woods ashtakiwa kwa shtaka la ajabu

Tuesday May 14 2019

 

By Mwandishi Wetu/AFP

"Uongozi una haki ya kumkataa mteja" ndivyo mabango kwenye baa nyingi yanavyoeleza. ingawa baa za kisasa hazina maandishi kama hayo.

Lakini ilani hiyo ndiyo itatumika kumshtaki mcheza gofu maarufu duniani, Tiger Woods baada ya muhudumu wa baa yake kunywa hadi kulewa na baadaye kufa kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha.

Ndugu wa marehemu huyo, wanadai kuwa muhudumu huyo anayeitwa Nicholas Immesberger, alihudumiwa pombe kupita kiasi, tovuti ya TMZ imeripoti juzi.

Wazazi wa Immesberger, ambaye alifariki Desemba mwaka jana akiwa na umri wa miaka 24, wamefungua kesi wakisema mtoto wao alikuwa akifanya kazi kama muhudumu kwenye baa ya The Woods in Jupiter, jimbo la Florida, na anamjua nyota huyo wa gofu, tovuti hiyo inayoandika habari za watu maarufu imeripoti.

Habari za nyota huyo kushtakiwa zilitokea saa kadhaa baada ya Woods kufanya mazoezi ya raundi ya pili kujiandaa na michuano ya 101 ya ubingwa wa PGA, ambayo ni ya pili mikubwa kwa mwaka. Michuano hiyo itafanyika Bethpage Black katika kisiwa, Long Island jijini New York.

Woods, ambaye alikaa miaka 11 bila ya kushinda taji lolote, aliondoa balaa hilo kwa kutwaa taji la michuano ya Masters mwezi uliopita na sasa anawania taji la 16 kubwa tangu aanze kushiriki mashi9ndano ya gofu. Alitunukiwa medali ya rais ya uhuru (Presidential Medal of Freedom) wiki iliyopita katika hafla iliyofanyika ikulu.

Meneja wa mgahawa huo, Erica Herman, ambaye ni mpenzi wa Woods, kwa mujibu wa TMZ, ndiye aliyemuajiri Immesberger kwenye mgahawa huo.

Kwa mujibuwa TMZ, Immesberger alimaliza zamu yake Desemba 10 lakini akaendelea kukaa kwenye baa hiyo kunywa na inadaiwa kuwa alihudumiwa kinywaji hadi kufikia kiwango cha kulewa chakari kabla ya kupelekwa kwenye gari lake.

Uongozi wa baa ulikuwa na haki ya kutoendelea kumhudumia kinywaji baada ya kuanza kuonekana kulewa.

Immesberger alishindwa kumudu gari lake jioni hiyo wakati akirudi nyumbani na kugonga. Alifariki katika ajali hiyo, kwa mujibu wa ripoti, ambayo pia inasema kiwango cha ulevi cha Immesberger kilifikia .256, ikiwa ni mara tatu zaidi ya kiwango kinachotakiwa.

Familia hiyo inadai kuwa Woods na Herman walijua kuwa Immesberger alikuwa na matatizo anapokunywa pombe, lakini wakamruhusu aendelee kuhudumiwa.

Advertisement