Tuhuma za rushwa ya Sh700,000 zamfikisha kortini Askari JWTZ

Wednesday June 26 2019

Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)

Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kutoka jeshi la Akiba Kinondoni,Johanes Kibambi akikabiliwa na shtaka la kupokea rushwa ya Sh 700,000 akipelekwa kwenye kizimba cha mahakama ya wilaya Kinondoni. Picha na Pamela chilongola 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), MT77341 Johanes Kibambi amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam kujibu shtaka la kuomba rushwa ya Sh700,000 ili aweze kumpatia Kelvin Fabiana nafasi ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Kibambi anayetoka ya mgambo wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam amefikishwa mahakamani leo Jumatano Juni 26,2019 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Takukuru, Vera Ndeoya amedai mbele ya mahakama hiyo Juni 17, 2019 katika ofisi za mgambo mshtakiwa akiwa mwajiliwa wa JWTZ aliomba rushwa kwa Fabian kama kishawishi cha kumpatia mafunzo aweze kujiunga na JKT.

Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa amekana shtaka linalomkabili.

Hakimu Mkazi, Caroline Kiliwa amesema mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili walioajiliwa kwenye sekta za umma au binafsi na wasiwe wa  JWTZ watakaosaini bondi ya Sh1 milioni.

"Hao wadhamini wawili msitoke JWTZ kwa kuwa huwa wanasumbua sana waje kutoka sekta za umma au binafsi na vitambulisho vinavyoletwa lazima tuvikague kwa makini kwa kuwa kunakuaga na udanganyifu itanilazimu niahirishe shauri hili," alisema Kiliwa.

Advertisement

Shauri hilo limeahirishwa hadi Juni 28,2019 litakapokuja tena.

Advertisement