UCHOKOZI WA EDO: Tumewaachia habari ya Bagamoyo, tunacheza bao maskani

Vuta taswira umesimama mahala ukiwa huna hili wala lile, ghafla akapita mtu mmoja akikimbia kwa kasi kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Baada ya muda akatokea mtu mwingine katika njia ileile aliyoingia jamaa wa kwanza anatoka kwa kasi kwenda kwingine.

Halafu ghafla akatokea mtu mwingine akakimbia kwa kasi kutoka kule alikotokea jamaa wa mwanzo na kukimbilia kule kule ambalo jamaa alikimbilia. Unabakia unashangaa. Nini kinaendelea? Unaanza kupatwa na wasiwasi yupi ambaye mbio zake zina tija?

Imetutokea juzi Watanzania. Awamu iliyopita ilikuja na ndoto za habari ya ule mradi wa Bagamoyo. Ikasisimua kusikiliza kilichomo katika mradi. Ghafla kwa sasa kuna Serikali nyingine na tunasikia ‘imefyekelea mbali’ mradi huo.

Saa chache baadaye, bosi wa mjengoni pale Dodoma akatupa maneno matamu kweli kweli kuhusu mradi huo wa Bagamoyo. Alikuwa katika ubora wake wa hali ya juu. Akapangilia hoja zake vema. Usingemtofautisha kati yake na yule kijana Mbunge wa Kigoma mjini. Akaona kuna kuna shida katika kuufuta huo mradi.

Sio siri, tulioishia darasa la saba tumeachwa njia panda. Utamu wa mradi ni mkubwa kwa kuusikiliza lakini hawa waliopo sasa sio wendawazimu. Labda kuna mambo mazito wamegundua. Kwamba mradi mnono kama huo unaweza kuufuta kwa sababu tu ‘hatutaki uwepo Bagamoyo’ haingii akilini. Inawezekana kuna jambo zaidi.

Hata hivyo Bosi wa Mjengo wa Dodoma naye anaposhindwa kuelewa chochote wakati yupo karibu na Serikali yake, sisi tulioishia darasa la saba tunachoka zaidi. Tunaishia kucheza bao tu. Tunawaachia wakubwa waamue kipi ni sahihi.

Walioamua mradi uwepo walikuwa na akili nzuri na wanaoamua usiwepo nao wana akili nzuri tu. Labda baadaye tutajua mengi zaidi lakini nyakati zitamuumbua mtu. Huu ndio uzuri wa nyakati. Huwa hazidanganyi.

Kwa sasa tumo mitaani tukicheza bao tu. Siku moja tutasikia habari nyingine ambayo itakuwa ‘hakimu’ wa habari zote kuhusu mradi wenyewe. Sisi tunasikilizia tu. Hatuna haja ya kuhukumu kwa sasa. Ni kama tumetazama mbio za huyu aliyepita kwa kasi kwenda huku, kisha mwingine akatokea njia ileile na kisha mwingine akatokea njia ileile.