UCHOKOZI WA EDO: Tupo darasani na ‘ticha’ wetu ni Profesa Kabudi

Unabaki kumtazama tu Profesa Kabudi na kisha kutabasamu. Namkubali. Ni moja ya vichwa vinavyofanya kazi sana. Niliishia darasa la saba kwa hiyo awali sikupata nafasi ya kufundishwa naye, lakini waliowahi kufundishwa naye wanasema jamaa ni ‘kichwa sana’.

Kwa bahati, hatimaye sasa nimebahatika kufundishwa naye. Hiki anachoendelea kutufanyia ni fundisho tosha. Hata wanafunzi wake wa zamani kwa sasa nao amewarudisha tena darasani. Ametuingiza darasani katika somo linaloitwa ‘mabadiliko ya mwanadamu’.

Niliyemsikia na kumuelewa ni tofauti na huyu lakini hata hivyo hili ni sehemu ya somo kutoka kwake. Kwa mfano, sasa anatufundisha kwamba kumbe ‘uprofesa’ bado ni jalala tu. Tulioishia darasa la saba tulidhani kwamba hii ni ngazi ya juu zaidi katika elimu. Kumbe hapana.

Profesa anaamini kwamba kabla ya kutinga geti la Ikulu kwenda kuapishwa alikuwa anaishi jalalani. Kumbe hata wale waliobaki pale Mlimani na kwingineko wako jalalani. Wakati ule namuangalia kwa husuda kubwa pale Mlimani City akila ‘lunch’ yake huku nikiwanong’oneza wenzangu ‘Profesa Kabudi huyo’ kumbe alikuwa jalalani? Kumbe alikuwa mavumbini? Nichukue fursa hii kumpa pole.

Siku moja akiachana na nafasi yake, zama zake zikiisha kule juu nadhani wanajalala wenzake watamkaribisha jalalani. Kwa sasa wamuache kidogo afunguliwe mlango wa V8. Mwanadamu anaishi mara moja tu. Nani anataka shida?

Profesa pia anatufundisha kwamba ndani ya mabadiliko ya mwanadamu unapaswa kuwa mpole. Ni kama alivyo sasa. Namba Moja ameweka wazi wakati mwingine huwa anamtukana Profesa tusi la chapchap la ‘mpumbavu’. Ni neno zito. Kama unabisha mwambie hivyo aliyekwambia kama atakubali.

Profesa akiambiwa hivyo anaendelea kuchapa kazi kwa nguvu. Maprofesa wa zamani wangefanya kile kitu kinachoitwa kulinda heshima binafsi. Kwa Kiingereza wasomi wakipita maskani kwetu huwa wanasema ‘to protect my dignity’. Wale wa zamani huwa wanaachia ngazi na kurudi shule kufundisha.

Profesa Kabudi anaendelea kuchapa kazi kwa utii mkubwa. Ni sehemu ya kujifunza kwetu katika somo hili la ‘mabadiliko ya mwanadamu’. Maisha yanakwenda kasi sana.