UCHOKOZI WA EDO: ‘Service’ za Bombardier ni kawaida tu kama chaguzi za marudio

Thursday January 17 2019

 

Hakuna cha kushangaa kwa kila kinachoendelea nchini. Mambo mengine ni ya kawaida sana. Tunapoteza muda kushangaa katika maswali ambayo majibu yake yanajulikana. Mfano ni kiasi cha Sh13 bilioni ambazo zitatumika katika ‘service’ (matengenezo) ya ndege zetu.

Mshangao na malumbano vilipaswa kuishia katika umuhimu wa ununuzi wa ndege zenyewe. Tulipaswa kumaliza ubishi, kukubali jinsi ya kuishi na ndege zenyewe. Ndivyo ilivyo. Moja kati ya gharama zake ni hizi za service. Naona watu wengi wanaweka michanganuo mitandaoni ya kujadili gharama hizi za marekebisho. Hapana, tuzikubali tu.

Ni kama tulivyokubali gharama za demokrasia. Tumeambiwa mbunge akijivua ubunge basi tunaitisha uchaguzi mwingine wa marudio hata kama mbunge yule yule atakwenda kugombea kwa chama kingine. Tunaambiwa hizo ndio gharama za demokrasia.

Inabidi tujiandae kisaikolojia kuishi na gharama hizi. Tunapoukubali mwanzo basi tuukubali ukatikati wake na tuukubali mwisho wake pia. Kuna mambo ambayo tungeweza kukata mzizi wa fitina na kubadili mwelekeo wa fikra zetu lakini tumegoma. Acha tugharamike.

Kwa mfano, nilidhani shirika letu lingeendeshwa kwa ubia na watu wengine “wenye nazo” ili Serikali au ATC ijitoe katika uendeshaji wa moja kwa moja na kujipanga kupokea gawio mwisho wa mwaka. Serikali haipaswi kufanya biashara. Tungeacha wabia waumize kichwa katika masuala haya. Tuliamua tulifanye hilo wenyewe sasa acha tuumize vichwa katika masuala kama haya ya Sh13 bilioni.

Ni kama ambavyo nilidhani tungeamua mbunge anayehama chama kimoja kwenda kingine angehamia na ubunge wake bila ya uchaguzi wa marudio. Hata hivyo, kwa sababu hatujaamua kuwa makini na fedha zetu nadhani acha tuzoee kuingia gharama. Ni kitu cha kawaida tu.

Advertisement

Tumetengeneza mfumo ambao tunatumia fedha halali katika matumizi ya gharama ya halali ni lazima na watawala wanaweza kutuonyesha risiti za matumizi. Ni kitu cha kawaida. Inahitaji roho ngumu kukubali lakini hakuna tunachoweza kufanya. Nje ya hapo ni uchochezi.

Nyakati zitaamua kama tunafanya uamuzi sahihi kwa sasa hasa baada ya kujinasibu kwamba tumedhamiria kubana matumizi. Vinginevyo kwa sasa tukubali tu kwamba tunafanya matumizi sahihi kwa sababu tunapatiwa risiti halali.


Advertisement