UCHOKOZI WA EDO: Kifo cha Fastjet kimekuja ghafla, hatukujiandaa vyema

Monday January 21 2019

 

Mke wa rafiki yangu amekwama Mbeya. Analazimika kurudi Dar es Salaam kwa kutumia usafiri wa basi. Siku hizi ni safari ya saa 13 barabarani. Mnatoka Mbeya saa 12 asubuhi, mnafika Dar es Salaam saa tatu usiku hilo linatokana na tochi nyingi barabarani na madereva sasa wanatii sheria.

Kwa mujibu wa mume wake, mke wake aliambiwa ndege ya ATCL imejaa mpaka Alhamisi. Nauli ya ndege anayo lakini analazimika kupanda basi bila ya kupenda. Tunaanza kulipia gharama za utawala wa shirika moja tu la ndege hewani. Kuna watu watatu waliwahi kuniambia wamekumbana na tatizo hilo.

Wakati huu tukiwa tumeifukuza Fastjet kwa majigambo huku Precision wakiwa hoi kwa muda mrefu, tuna shirika moja tu la ndege, ATCL. Wamepewa nguvu sokoni lakini sioni kama wamejiandaa kukidhi mahitaji ya abiria.

Ndege kubwa tatu ambazo zimenunuliwa inabidi zipige safari za mbali. Haziwezi kwenda Mbeya au Mwanza. Kibiashara ni hasara. Inabidi ziende Hong Kong, Dubai, China, Marekani, India na kwingineko. Humu ndani inabidi zitumike zile mbili ndogo.

Kinachofuata kwa sasa ni kama kile kilichomtokea mke wa rafiki yangu. Una fedha yako mfukoni lakini unakosa huduma. Wale watu wa Mwanza wakati ule kulikuwa na ndege tatu kwa siku. Asubuhi, mchana na jioni. Leo wana Bombardier tu ambayo wakati inajipanga kwenda Mwanza mara mbili kumbuka bado kuna safari za Mbeya, Kiimanjaro, Tabora na Dodoma zinawasubiri.

Abiria wote wa Fastjet wamehamia ATCL, hapo kumbuka kuna abiria wa ATCL ambao tayari walikuwepo kabla ya kukata roho kwa Fastjet. Maisha yanaanza kuwa magumu.

Ndege zetu tunazipenda sana na tunamuunga mkono Namba Moja katika juhudi zake za kufufua shirika hili, lakini nadhani walipaswa kuwa na upinzani hewani. Usafiri wa Ndege sio biashara tu, ni huduma. Kama unalazimika kusubiri wiki nzima upate nafasi katika ndege basi kuna tatizo kubwa tumelitengeneza.

Asiyetamani shirika letu lifufuke ni mchawi, lakini lazima tuwe wakweli na tatizo ambalo tunalitengeneza kwa sasa. Ni wakati mwafaka wa ndege zetu kupiga fedha ndefu lakini bado kuna fedha nyingi wanaziacha ardhini. Kifo cha Fastjet ni tatizo kwetu.


Advertisement