UCHOKOZI WA EDO: Wakati sahihi wa kumsamehe Mzee Pinda umefika

Wednesday January 16 2019Edo  Kumwembe

Edo  Kumwembe 

Sura yangu inaweka tabasamu ninapofikiria uchanga wa nchi yetu. Tulipata uhuru mwaka 1961, lakini usidhani ni mbali sana, hapana, nchi yetu bado changa. Bado haijapitia mengi kama tulivyofikiria. Mwaka huo wengine tulikuwa hatujazaliwa lakini kwa sasa sisi na wazee wetu tunashuhudia mengi kwa pamoja.

Najaribu kuwaza kauli kali za utawala uliopita. Moja kati ya kauli kali ilitolewa na Mzee Mizengo Pinda. Alikuwa Waziri Mkuu wetu. Alhamisi moja pale Dodoma alijikuta akijibu swali fulani katika namna iliyowaacha wengi na mshangao. Nadhani hata yeye mwenyewe anajisikia vibaya mpaka leo.

Ni kuhusu madai ya watu wa Mtwara kutandikwa na wanajeshi wakati wa maandamano ya kudai haki yao kuhusu gesi kutotolewa kusini kuletwa Dar es salaam. Alisikia akisema ‘wapigwe tu, maana hamna namna nyingine, watapigwa tu’.

Nchi ilipigwa na butwaa. Kinywa cha Waziri Mkuu kilikuwa kinatoa maneno mazito ya kutisha. Mtu mwenyewe alizoeleka kwa kuwa mtulivu na mwenye busara. Kwa Tanzania ilikuwa kitu kigeni. Mpaka wakati anaondoka madarakani hatukumsamehe Mzee Pinda.

Leo tunapotazama nyuma na kuikumbuka kauli ya Mzee Pinda tunagundua kwamba ilikuwa kauli ya kawaida tu kama angeitoa katika zama hizi. Kauli yake imeondolewa na uzito na kauli nyingi nzito ambazo zinatawala katika zama hizi.

Kuna wale walioambiwa wangepigwa wao na ndugu za wazazi wao. Kuna yule bosi wa mkoa kijana ambaye damu yake inachemka. Aliwahi kutamba katika kikao cha watu wazima wenye umri wa baba yake kwamba angewachapa viboko kama wangekuja na mabango ya kudai haki zao mbele yake.

Kila siku unatazama taarifa ya habari au kusoma mitandaoni jinsi kauli za kibabe zinavyotolewa na wakuu wa wilaya au mikoa. Unaishia kutabasamu tu. Siku moja Namba Moja alitukumbusha kwamba viongozi wake hasa vijana tuwasamehe kwa sababu damu zinachemka. Huwa natabasamu kila ninapokumbuka jinsi ambavyo Watanzania wamesahaulishwa ile kauli ya Mzee Pinda na kauli kali za zama hizi. Ubaya haufutwi na ubaya, lakini nadhani ni wakati wa kumsamehe Mzee Pinda. Tumwache alime kwa amani popote alipo.

Ni kweli alikosea lakini ni katika nyakati kama hizi tunakumbushwa uchanga wa taifa letu, kwamba bado tuna mambo mengi ya kuona na kusikia kutoka kwa wanaotutawala. Binafsi sina kinyongo naye. Nimesikia mengi baada ya kauli yake ile.

Advertisement