Uamuzi mzuri unaoibua maswali kuhusu yajayo ya zao la korosho

Muktasari:

Uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuingilia mauzo ya korosho kwa kupanga bei ya Sh3,300 kwa kilo bila kuwa na makato yoyote, umepokelewa kwa furaha kubwa na wakulima ambao wameuona kuwa huo ni uamuzi mzuri na neema kwao.

Dar es Salaam. Uamuzi wa Serikali kuingilia mauzo ya korosho kwa kupanga bei ya Sh3,300 kwa kilo bila kuwa na makato yoyote, umepokelewa kwa furaha kubwa na wakulima ambao wameuona kuwa huo ni uamuzi mzuri na neema kwao.

Hata hivyo yapo mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi kwa faida ya siku zijazo kwa wakulima, maendeleo ya zao hilo na jamii kwa ujumla. Mwananchi limebaini.

Wakati ulipaji ukiendelea kwa wakulima japo kwa kasi ndogo, vyama vya ushirika vya msingi na vikuu pamoja na halmashauri za wilaya vimebaki njia panda zisijue pa kupata fedha za kujiendesha

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Newala, Mussa Simaye alisema kwa sasa wanasubiri tamko la Serikali kwani kwa bei ya Sh3,300 hawatarajii kupata ushuru wa korosho.

“Kwa msimu wa mwaka jana tulipata ushuru wa korosho wa zaidi Sh800 milioni. Kwa mfuko wa elimu tulipata Sh356 milioni kwani wakulima huchangia baada ya kuuza korosho,” alisema Simaye.

Akifafanua zaidi, Simaye alisema mapato hayo hupatikana kutokana na mjengeko wa bei ambapo halmashauri hupata asilimia 3 katika bei elekezi ambayo mwaka jana ilikuwa Sh1,400. “Si kwamba tumekosa kabisa, kwa sababu hatujapata tamko la Serikali mpaka sasa,” alisema.

Akifafanua matumizi ya fedha za makato ya korosho, Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmed Katani alisema kuna mfuko wa elimu uliokuwa ukitengewa fedha.

“Wilaya yetu ina kata 31 na kuna shule za sekondari 28 katika kata hizo, kwa hiyo tulichofanya kwanza ni utekelezaji wa agizo la Rais mstaafu Jakaya Kikwete la kujenga maabara kwa kupeleka Sh10 hadi 15 milioni kwa kila shule,” alisema Katani.

“Hata Rais (John) Magufuli alipoagiza tuweke madawati shule tulichangia zaidi ya Sh300 milioni kutoka kwenye fedha za korosho,” aliongeza.

“Kimsingi maendeleo yote ya wilaya hii yanategemea makato ya korosho, hata barabara ya lami, huduma za afya huwa tunachangia. Ruzuku ya Serikali inachelewa na ikija ni kama asilimia 40 ya bajeti ya mwaka ya halmashauri,” alisema.

Mbali na Tandahimba, Wilaya ya Nachingwea nayo iko njia panda. Mbunge wa jimbo hilo, Khamis Masala alisema kutokuwepo makato katika bei ya Sh3,300 kutawanyima jumla ya Sh1.4 bilioni walizokusudia kukusanya kwa ajili ya mfuko wa elimu na mapato ya halmashauri.

“Sisi kama halmashauri tuna mfuko wa elimu ambao kwa msimu wa 2017/18 tulikusanya Sh600 milioni tunazotumia kuongeza kwenye sekta ya elimu. Halmashauri ilikusudia kukusanya Sh800 milioni, sasa haitapatikana. Hatujapata maelekezo yoyote, tunasubiri kujua fedha hizo zitapatikanaje,” alisema.

Kuhusu malipo kwa wakulima, Masala alisema licha ya Serikali kusema inalipa lakini zoezi linakwenda taratibu.

“Mpaka sasa wilaya hii kuna vyama 34, kati yake 15 vimehakikiwa ni sita tu vimelipwa. Wakulima wamekopa fedha benki na kwa watu binafsi hawajui watalipaje wala wataandaaje mashamba yao kwa msimu mwingine,” alisema.

“Watu wanauza korosho kwa Kangomba kwa sababu ya njaa na ili kununua pembejeo. Mwaka jana Serikali ilitoa pembejeo bure na mwaka huu mfuko wa mbolea wa kilo 50 umeuzwa Sh70,000 hali iliyowafanya wauze korosho ili kulipa madeni ya mikopo ya pembejeo. Kama Serikali inataka kudhibiti Kangomba ilete pembejeo kwa wakati,” alisema.

Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alikuwa akisisitiza suala la kuwalipa kwanza wakulima na kisha wataangalia madeni ya waau walioshiriki vikiwemo vyama vya ushirika, wasafirishaji, wabebaji na halmashauri za wilaya.

“Sisi kazi yetu tunayofanya ni kumlipa na wewe kama unajua unamdai umfuate huko. Tusingependa tusikie mara nini, sisi tunataka kwanza apate hela yake,” alisema Waziri Hasunga akiwa Newala hivi karibuni.

Pia alisema kutokuwepo makato kutaathiri uendeshaji wa vyama vya ushirika.

Malalamiko kama hayo pia yametolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, Abou Mjaka akisema walitarajia kukusanya Sh280 milioni kutoka kwenye makato ya korosho.

“Tulitarajia kupata Sh280 milioni msimu huu ambazo tungetumia kwenye elimu. Tunataka kujenga madarasa 14 na kila darasa linagharimu Sh20 milioni, lakini hadi sasa hatujui tutazipataje. Fedha nyingine zinaingia kwenye bajeti ya halmashauri kuongezea,” alisema Mjaka.

Vyama vya ushirika navyo vina hofu ya kupoteza malipo yao kufuatia mfumo huo mpya. Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Tandahimba na Newala (Tanecu), Mohamed Nassoro alisema chama hicho kilitarajia kukusanya Sh3 bilioni baada ya kukata Sh30 kwa kila kilo katika tani zaidi ya 100,000 walizokusanya.

Alisema wameshazungumza na Waziri wa Kilimo, na Mrajisi wa vyama vya ushirika lakini hawajapata mwafaka