Uamuzi wa Maalim Seif wamuibua Mbowe

Muktasari:

  • Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania, Freeman Mbowe amesema hatua ya Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia chama kingine cha siasa ni moja ya njia ya kuendeleza mapambano ya kisiasa

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kilichotokea kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia Chama cha ACT- Wazalendo ni sehemu ya mapambano.

Mbowe amesema hayo leo Jumatatu Machi 18, 2019 ikiwa ni muda mfupi kupita tangu Maalim Seif autangazie umma wa Watanzania kuwa yeye, viongozi na wanachama wa chama hicho wanaomuunga mkono wanahamia ACT- Wazalendo.

“Maalim na timu yake bado ni sehemu muhimu sana katika mapambano haya, tunawatakia kila la kheri,” amesema Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania.

Licha ya kuwatakia maisha mema huko ACT- Wazalendo lakini amewaomba wakafanye siasa kuanzia ngazi za chini ili kuhakikisha malengo ya kuwapigania wananchi yanafikiwa.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi, Mbowe amezungumzia kwa nini anafurahia Maalim Seif na wenzake kwenda ACT- Wazalendo, lakini ACT- Wazalendo watapokewa kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)? Yote haya usikose gazeti la Mwananchi kesho Jumanne Machi 19, 2019