Udanganyifu watajwa usajili laini za simu

Muktasari:

Usajili wa laini za simu kwa kutumia kitambulisho cha Taifa umetajwa kugubikwa na udanganyifu unaofanywa na mawakala wa mitandao mbalimbali ya simu nchini Tanzania


Mwanza. Usajili wa laini za simu kwa kutumia kitambulisho cha Taifa umetajwa kugubikwa na udanganyifu unaofanywa na mawakala wa mitandao mbalimbali ya simu nchini Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Julai 10, 2019 mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo amesema baada ya kupata taarifa za kuwapo matapeli wameanza operesheni ya kuwasaka na kuwakamata wanaokiuka sheria kwa kusajili laini wanazoiita ‘take away’.

“Kumeibuka utapeli, kwanza wapo baadhi ya mawakala wanasajili laini zaidi ya moja wakiita ‘take away’ kwa kutumia kitambulisho cha mtu mmoja halafu nyingine wanakuja kuziuza kwa watu wasio na kitambulisho cha Taifa jambo ambalo ni kosa,”

“Pia tumegundua baadhi wanatumia ujanja kupata namba za siri za mteja wakati wakisajili kama anakuwa na fedha wanaitoa,” amesema.

Amesema ni marufuku kwa mtu yeyote kuuza na kusambaza au kusajili laini za simu bila kuwa uthibitisho kutoka kwa mtoa huduma.

Mhandisi mwandamizi wa mamlaka hiyo Kanda ya Ziwa, William Mnyippembe amesema hadi sasa wamewakamata watu 12 waliokutwa wakiendesha shughuli hiyo bila kufuata utaratibu.