Udart inavyoweza kushusha nauli ya ‘Mwendokasi’ kwa kutumia gesi

Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam (Dart), ulianza rasmi Mei 10, 2016 kabla ya kuzinduliwa Januari 25, 2017 na Rais John Magufuli aliyewataka viongozi wasimamizi kuhakikisha faida inapatikana katika uendeshaji wake.

Unatoa huduma katika njia nane, vituo vikuu vitano, vituo vidogo 28 kwa kutumia mabasi 140 na hujumuisha mabasi makubwa 39 yenye uwezo wa kubeba abiria 160 kila moja na mabasi madogo 101 yenye uwezo wa kubeba abiria 60 kila moja.

Mradi huo wenye urefu wa kilomita 20.9, una thamani ya Sh403.5 bilioni, zilizotokana na mkopo wa Sh317 bilioni kutoka Benki ya Dunia huku Serikali ikitoa Sh86 bilioni.

Licha ya faida nyingi za kiuchumi kupitia mradi huo, Serikali inasema inategemea faida kupitia biashara chini ya Kampuni ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), inayokadiria kuwa na idadi ya abiria takribani 200,000, wanaotumia usafiri huo kwa malipo ya Sh650 kwa kila tiketi ya mzunguko wa njia.

Kwa makadirio hayo ya Udart, abiria hao ni sawa na makusanyo ya wastani wa Sh130 milioni kwa siku.

Msemaji wa Udart, Deus Bugaywa anasema idadi ya mabasi yanayotumika kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa ni 126 ambayo hutumia lita 16,500 kwa siku. Jumamosi hutumia lita 13,000 na Jumapili lita 12,000 sawa na wastani wa lita 15,357 zinazotumika kila siku.

Kwa mujibu wa makadirio ya bei yaliyothibitishwa na Ewura (Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Nishati na Maji), kwa miezi minne iliyopita, wastani wa bei ya jumla ya Dizeli kwa Jiji la Dar es Salaam ni Sh2,157. Hii inamaanisha kuwa Udart huenda ikawa inatumia wastani wa Sh33.13 milioni kununua lita 15,357 kwa siku, sawa na wastani wa Sh993.7 milioni kwa mwezi.

Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani ameiagiza TPDC kupitia Kampuni yake tanzu ya Gasco kuhakikisha wanatumia fursa hiyo ya kuanzisha vituo vya kujaza gesi katika mabasi yaliyopo chini ya mradi wa Dart. Kalemani anasema itasaidia kupunguza gharama na kuokoa mazingira.

“TPDC na Gasco mjipange kuhakikisha Udart hata daladala ziunganishwe kwenye matumizi ya gesi, hadi sasa kuna magari 200 yameshaunganishwa na gesi,” anasema Waziri Kalemaji wakati wa ziara yake katika mradi ya usambaji wa gesi majumbani maeneo ya Mikocheni, Chuo Kikuu, Mlalakua na Kiwanda cha Coca cola.

Meneja wa Usambazaji Gesi Asilia kutoka Ewura, Mhandisi Thobias Rwelamila anasema mradi huo utaokoa fedha nyingi zinazotumika katika ununuzi wa mafuta ya kuendeshea mabasi hayo.

Kanuni za bei ya gesi asilia za mwaka 2016, zinaonyesha kuwa matumizi ya gesi hiyo katika magari itasaidia kuokoa asilimia 40 ya gharama inayotumika katika ununuzi wa lita moja ya Petroli na Dizeli ya wakati husika.

“Pungufu ya gharama za mafuta ni asilimia 40 kwa hiyo gharama zitapungua sana kwa mradi huo,” anasema Rwelamila.

Kwa makadirio hayo ya kikanuni, pungufu ya asilimia 40 katika wastani wa Sh900 milioni inayotumika katika ununuzi wa dizeli kwa mwezi, ni sawa na wastani wa Sh397.5 milioni.


Mazungumzo yameshaanza

Kwa mujibu wa wizara ya nishati, tayari Serikali imetenga kiwango cha futi za ujzo trilioni moja ya gesi asilia kwa ajili ya kuunganisha nishati ya kupikia majumbani, trilioni 3.8 kwa ajili ya viwandani, trilioni 4.6 kwa ajili ya viwanda vya mbolea na ‘petrol chemical’ na trilioni 9.1 kwa ajili ya kuzalishia umeme.

Mkurugenzi Mkazi Kanda ya Afrika wa Shirika la Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang’ anasema matumizi ya gesi asilia kwenye magari ni nafuu, huokoa gharama na hutunza mazingira, akishauri TPDC kuimarisha mradi wa kujaza gesi kwenye magari.

Hata hivyo, hadi sasa Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), lina kituo kimoja tu cha kujaza gesi asilia kwenye magari, kipo Ubungo Maziwa Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa TPDC, vituo vya kujaza gesi kwenye magari vinatarajia kuongezeka mara tu mradi wa usambazaji gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara utakapokamilika.

Mkurugenzi wa Biashara za Mafuta na Gesi, wa Kampuni hiyo ya Mafuta, Mhandisi Emmanuel Gilbert anasema tayari kampuni hiyo ya Serikali imeshafanya majadiliano na Dart kwa ajili ya kuanzisha mradi utakaogharimu Sh5.5 bilioni ili kutoa huduma ya gesi kwenye mabasi hayo.

Gilbert anasema mradi huo utakapokamilika Juni mwakani, utajengwa katika eneo la Kituo cha Mabasi ya Mikoani Ubungo, baada ya kuhamishwa. Anasema hatua inayoendelea kwa sasa ni ununuzi na mradi huo utawezesha mabasi 214 kujazwa gesi kwa siku moja.

“Tumeshazungumza nao katika majadiliano ya awali, kazi itaanza Agosti mwaka huu na kituo kitakuwa kimekamilika ifikapo Juni mwaka ujao, kila basi litajazwa baa (kipimo cha ujazo wa gesi) kati ya 190 hadi 195, gharama zitapungua kwa asilimia 40 ya mafuta,” anasema.

Gilbert anasema mshauri mwelekezi wa mradi huo atafanya tathmini ya mradi ikiwamo ulaji wa mafuta kwa mabasi hayo, umbali wa safari zake kabla ya kushauri usimikaji wa kituo cha kujaza gesi katika eneo hilo na kwamba kiwe na uwezo gani.

Bugaywa anasema tayari Dart imeshawasiliana na watalaamu wa Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa gharama zitakazopungua katika uendeshaji wa mradi huo.


Uwezekano wa kushusha bauli

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Josephat Kandege, anasema matumizi hayo ya gesi katika mabasi ya Udart yatasaidia kupunguza hata kiwango cha nauli kinachotozwa sasa kwa kuwa gharama za uendeshaji zitapungua.

Kandege anasema matumizi ya gesi ni busara itakayopunguza gharama kubwa za uendeshaji, itaepusha uharibifu wa mazingira na kuondoa uchakachuaji wa mafuta unaoharibu magari.

Awali, Rais Magufuli aliagiza viongozi kuhakikisha mradi huo unatengeneza faida katika utekelezaji wake ili kuanzisha miradi mingine katika jiji hilo.