Ufunguzi masoko ya tumbaku kufanyika leo

Kaimu mwenyekiti wa bodi ya tumbaku nchini,TTB,Hassan Wakasuvi,akizungumza katika ufunguzi wa masoko ya tumbaku mjini Urambo leo.picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

Kaimu mwenyekiti wa TTB amewalaumu viongozi kwa kuchangia changamoto zinazowakumba wakulima sokoni

Tabora. Tabia ya viongozi kushindwa au kuzembea kutembelea maeneo yanayolimwa zao la tumbaku kunasababisha kuchelewa kutatuliwa kwa changamoto zinazowakabili wakulima.

Akizungumza katika ufunguzi wa masoko ya tumbaku leo Jumatatu Mei 13, 2019 mjini Urambo unaotarajiwa kufanywa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, kaimu mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), Hassan Wakasuvi amesema wakulima hunyanyaswa kama viongozi hawatembelei masoko.

Amesema viongozi wanapotembelea hata wateuzi wa tumbaku hushindwa kuwaonea wakulima kwa kuwapa bei ndogo kwa kisingizio cha kutokuwa na ubora.

Ametoa mfano wa yeye mwenyewe, kutembelea masoko ya tumbaku yaliyoanza mwanzoni mwa mwezi huu katika baadhi ya maeneo nchini.

Amebainisha kuwapo baadhi ya kasoro kama wakulima kutopewa bei nzuri kutokana na tofauti ndogo ya rangi katika majani ya tumbaku.

Amesema tofauti inaweza kuonekana ndogo lakini mwisho mwa wa siku, mkulima anapata bei ndogo.

Kaimu mkurugenzi wa TTB, Dk Julius Ninga amesema watatekeleza maelezo yote yanayotolewa na Serikali.

Amesema tumbaku itakuwa imenunuliwa ifikapo Julai mwishoni, mwaka huu.