Ugonjwa kimeta waua watu wanne Songwe, Serikali yatoa tahadhari

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile

Muktasari:

  • Taarifa za awali za mlipuko wa ugonjwa wa kimeta mkoani Songwe zilitangazwa Januari 3 na hadi sasa mbali na watu wanne kufariki, wengine 81 wanaugua ugonjwa huo baada ya kula nyama ya ng'ombe aliyekuwa na maradhi hayo.

Momba/Dar. Watu wanne, wakazi wa Kijiji cha Nzoka, Wilaya ya Momba mkoani Songwe wamefariki dunia kwa ugonjwa wa kimeta.

Jumla ya watu 81 wameugua ugonjwa huo baada ya kula nyama ya ng’ombe aliyekuwa na ugonjwa huo.

“Tumechukua hatua kwa kukusanya sampuli na kudhibitisha kuwapo wa ugonjwa wa kimeta,” Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile aliiambia Mwananchi jana, “Mpaka (leo) jana, hakuna ongezeko la wagonjwa wapya na waliopo wameshapatiwa matibabu.

“Januari 3 tulipata taarifa ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa huu katika Kijiji cha Nzoka na mpaka sasa taarifa zilizopo ni kwamba wagonjwa 81 waligunduliwa na kati yao wanne wamefariki.”

Dk Ndugulile alisema taarifa walizopata kutoka Songwe ni kwamba wananchi waliuziwa nyama kwa bei ya Sh500 kwa kilo na baada ya kula waliugua ugonjwa huo.

Kwa kawaida kilo moja ya nyama katika eneo hilo ni Sh4,000 lakini nyama iliyosababisha maradhi hayo iliuzwa kwa mapande ambako kila moja liliuzwa kwa Sh500 kutokana na mifugo mingi kufa.

Dk Ndugulile alitoa tahadhari kwa wananchi, “Waache mara moja kununua nyama ambayo hawajui chanzo chake. Lazima ukae uhoji, wananchi waende kununua nyama katika bucha zilizodhibitishwa na Serikali.”

Alisema kwa sasa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo inaangalia namna ya kutoa chanjo kwa mifugo katika eneo hilo ili kuondoa kabisa vimelea vya ugonjwa huo kwa wanyama.

“Bado tunaendelea kutoa elimu kwa waathirika wa ugonjwa huu. Wawakilishi wetu wamekuwa wakitoa elimu hii maeneo ya mikusanyiko ya watu na wale wanaopatiwa matibabu hospitalini,” alisema.

Mganga mkuu Wilaya ya Momba Dk Anno Masseta alisema baada ya kuthibitika kuwa ugonjwa huo ni kimeta ambao unatokana kula nyama iliyoathirika, wananchi wameelimishwa kutokula mizoga, kunywa maziwa ya ng’ombe aliyeathirika na mnyama akifa kwa maradhi hayo afukiwe au achomwe moto.

Alisema sampuli nne zilichukuliwa na majibu ya sampuli mbili yalionyesha vimelea vya kimeta.

Awali, mkuu wa Wilaya ya Momba, Jumaa Irando alisema mwanzoni mwa mwaka huu watu 74 waliripoti katika vituo vya kutolea tiba wakiwa wanaugua ugonjwa huo.

Alisema watu hao wanahofiwa walikula nyama ya ng’ombe aliyeathirika Desemba 25 mwaka jana, siku ambayo alisema watu wengi walikula nyama ambayo haijafanyiwa uchunguzi na daktari wa mifugo.

Irando alisema wakati taarifa hiyo inatolewa na diwani wa kata hiyo, Credo Simwinga, tayari watu hao walikuwa wamezikwa na kwa mujibu wa maelezo ya wenyeji, marehemu hao walionyesha dalili sawa na za wagonjwa waliopo.

Alisema ili kudhibiti maradhi hayo, tayari zaidi ya lita 25,000 za dawa ya chanjo zimepelekwa kijijini hapo ili kuchanja mifugo yote na kuwa katika kipindi hicho hakuna mnyama yeyote atakayechinjwa na kuwa hata baada ya hapo wananchi wameelimishwa kuacha ulaji wa mizoga na wahakikishe nyama yote inapimwa na mganga wa mifugo.

Simwinga alisema watu wote waliofariki waliugua ugonjwa sawa na wagonjwa wengine ambao wamelazwa katika vituo vya tiba na hivyo kufanya waamini kuwa wagonjwa hao walipata maambukizi ya kimeta kama ilivyoonyesha katika vipimo vya madaktari.

Alisema ng’ombe walianza kufa katika kata yake tangu Novemba, mwaka jana na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu waliwauzia wananchi nyama hiyo ambayo pia haikupimwa na ofisa mifugo.

Simwinga alisema kuanzia jana shughuli ya chanjo ya mifugo iliyosalia inaendelea na wametoa agizo kuwa ni lazima kila mwenye mifugo achanje na maofisa mifugo wameagizwa kusimamia zoezi hilo ipasavyo.

Mkazi wa Nzoka, Samwel Malya (Manji) akizungumza na Mwananchi kwa simu alisema maradhi hayo yanatokana na tabia ya wakazi wa eneo hilo kula mizoga inapokufa huku nyama hiyo ikiwa haijapimwa na wataalamu wa afya.

Ushuhuda wa mgonjwa

Mmoja wa waathirika wa ugonjwa huo, Michael Simtanda alisema alianza kuona upele uliojitokeza katika mkono wake wa kushoto ambao unafanana na jereha la kuungua moto na alipojikuna ulipasuka na siku iliyofuata mkono mzima ulivimba hali iliyomfanya aende hospitali.

“Ni kweli tulikula nyama ya ng’ombe aliyekufa. Kuanzia Novemba mwaka jana, ng’ombe wengi walikufa na ilipofika Januari 4, watu walianza kuugua ugonjwa wenye dalili kama niliougua mimi na nilipoona hivyo nilikwenda hospitali haraka.