Uhuru azuia chupa za plastiki Kenya

Muktasari:

Miaka miwili baada ya kuzuia mifuko ya plastiki, Rais Uhuru Kenyatta amekwenda hatua zaidi kwa kutangaza marufuku ya chupa za plastiki kuanzia Juni 5, mwakani.


Canada. Miaka miwili baada ya kuzuia mifuko ya plastiki, Rais Uhuru Kenyatta amekwenda hatua zaidi kwa kutangaza marufuku ya chupa za plastiki kuanzia Juni 5, mwakani.

Akizungumza katika Kongamano la Wanawake linaloendelea nchini Canada, Rais Kenyatta alisema marufuku hiyo itahusu chumba za plastiki ambazo hutumika mara moja.

“Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira zinapatikana Kenya na taifa letu limekuwa likiendesha kampeni ya utunzaji wa mazingira. Miaka miwili iliyopita tulipiga marufuku utengenezaji, matumizi na uuzaji wa mifuko ya plastiki. Leo (Jumatano) natangaza matumizi ya chupa za plastiki ambazo hutumiwa mara moja,” alisema.

Alisema marufuku hiyo pia itatekelezwa katika maeneo yenye ulinzi kama vile mbuga za kitaifa, fukwe za bahari, misituni na maeneo ya uhifadhi.

Rais Kenyatta alitoa tangazo hilo kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Ulimwenguni iliyofanyika sambamba na kongamano hilo.

Rais alitoa wito kwa wanawake na wasichana kukumbatia kampeni hiyo kwa sababu wao ndio huathiriwa zaidi na shughuli za uharibifu wa mazingira.

“Kampeni za uhifadhi wa mazingira ziliongozwa na mwanamke mmoja Mkenya, Profesa Wangari Mathai, ambaye alipewa tuzo ya Nobel kwa juhudi hizo mwaka 2004. Heshima hii ilitokana na juhudi zake katika kutetea masuala ya uhifadhi wa mazingira na haki za wanawake,” akasema Rais Kenyatta

“Utunzaji wa mazingira huwezesha kujengwa kwa jamii yenye afya na inayoweza kuzalisha mali. Hii ndiyo maana wanawake na wasichana ambao ndio waathiriwa wakuu wa uharibifu wa mazingira sharti wawe mstari wa mbele katika kampeni hizi,” akaongeza.

Februari 28, 2017, Serikali ilizuia matumizi, utengenezaji na uuzaji wa mifuko ya plastiki kama hatua ya kuhifadhi mazingira.

Hatua kama hiyo imetekelezwa na Tanzania huku ikiwa tayari imetekelezwa na mataifa mengine ya Afrika kama Rwanda, Mauritania na Eritrea.