Uislamu unavyoamrisha waumini kufanya kazi

Friday February 8 2019

 

By Sheikh Muhammad Idd

Uislamu ni dini inayotambua na kuthamini umuhimu wa mali. Bila ya mali Muislamu hawezi kutekeleza ibada za Hijja, Zaka, kutoa sadaka, kulea yatima na wajane, kujenga misikiti, shule vituo vya afya na mambo mengine kadhaa ya kimaendeleo.

Uislamu unamtambua mwenye mali kwamba anazo ibada zaidi ambazo anaweza kuzifanya kuliko yule ambaye hana mali.

Kutokana na umuhimu mkubwa wa mali, Uislamu unamtambua Muislamu ambaye ameuawa wakati wa zoezi la kutetea mali yake asinyang’anywe kuwa amekufa akiwa ni miongoni mwa Mashahidi (watu wanaiopata ujira mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu).

Kuna njia nyingi za kupatia mali lakini njia bora kuliko zote ni mtu kufanya kazi akapata mali kutokana na jasho lake. Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Hakika bora ya chumo ni chumo la mtu linalotokana na mkono wake (kazi yake)”

Akafafanua zaidi Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) akasema: “Mwenyezi Mungu anampenda mja mwenye kufanya kazi na yeyote mwenye kuhangaikia familia yake anakuwa ni kama anayepigana jihadi katika Dini ya Mwenyezi Mungu” Akaongeza tena akasema: “Hakika katika madhambi kuna madhambi ambayo hayafutwi na swala wala sadaka wala Hijja na inayafuta madhambi hayo ile tabu anayoipata mja katika kutafuta maisha yake”.

Kutokana na umuhimu huo wa kufanya kazi ili kila mja apate riziki yake ya halali, akatufundisha Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) akatuambia: “Mkimaliza kuswali Alfajir msilale mkaacha kwenda kutafuta riziki zenu”.

Uislamu haukuishia tu kuelekeza na kufundisha umuhimu na ulazima wa kufanya kazi bali Uislamu umeelekeza mfumo wa kazi na ujira. Uislamu umemuelekeza mwajiri kwamba Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amekataza kumpa mtu kazi yoyote mpaka kwanza ujira wake uwe wazi. Habari ya mapatano kwamba muajiriwa afanye kazi halafu mapatano ya ujira wake yawe baada ya kazi, hilo halikubaliwi na Uislamu.

Uislamu umemuelekeza mwajiri pia kwamba baada ya kukamilika kazi ule ujira waliokubaliana na mwajiriwa usicheleweshwe na ulipwe kwa mujibu wa makubaliano.

Anasema Mtume rehma zimshukie: “Kumdhulumu mfanyakazi malipo yake ni miongoni mwa madhambi makubwa”;

Akamalizia Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) kwa kusema: “Mpeni mfanyakazi ujira wake kabla halijakauka jasho lake”.

Nidhamu ya kazi

Pia Uislamu umeelekeza kwamba katika kufanya kazi kuna nidhamu. Miongoni mwa nidhamu za kazi ni kutomuadhibu mfanyakazi kwa kosa ambalo limefanyika kwa bahati mbaya bila ya uzembe wake.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Msiwapige watumishi wenu kutokana na kuvivunja vyombo vyenu hakika vina hivyo vyombo ajali kama ajali za watu”. Hapo tunapata mafunzo kwamba makosa yote ya bahati mbaya hatakiwi muajiri kutoa adhabu.

Kanuni nyingine ya nidhamu ya kazi inayoelekezwa na Uislamu ni mfanyakazi kuwa muadilifu na mkweli kwa mwajiri wake na ajue kwamba kwa dhulma yoyote anayomfanyia mwajiri wake, hayo hayatoishia hapa duniani kwani kwa hakika kesho (Siku ya Hukumu) ataulizwa mbele za Mwenyezi Mungu na atapoteza thawabu nyingi atakazonyang’anywa na Mwenyezi Mungu kama fidia ili kumlipa mwajiri aliyedhulumiwa.

Amesema Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam): “Na mtumishi (mfanyakazi) ni mchunga katika mali ya bwana wake na yeye ataulizwa juu ya uchungaji wake”.

Kutokana na muktadha wa yote, kufanya kazi ni wajibu kwani ndio njia ya kupatia kipato, kipato ambacho kitamsaidia mtu kujikimu, kuikimu familia yake na kutenda mema yanayomridhisha Mola Muumba ambayo yanahitaji mali na bila ya mali hayatendeki kama vile kutoa Zaka na sadaka.

Njia za kupata mali

Umuhimu na ulazima wa kufanya kazi unatimia zaidi pale ambapo mwanaadamu anahitajia matumizi ya lazima kama vile mavazi, makazi, chakula, matibabu na kadhalika, na yote hayo yanahitajia mali. Na mwanaadamu anaweza kupata mali kwa njia tatu:

Kurithi. Mwanaadamu anaweza kurithi mali kutoka kwa wazazi wake. Sio vyema mtu kubweteka na kulemaa eti akisubiri wazazi wake wafe ili arithi mali apate kuendesha maisha yake kwa mali ya kurithi, na hata akiipata hiyo mali ya mirathi kama hana ‘akili’ ya kuiendeleza itakwisha yote. Njia nzuri ya kupata mali ni kujituma ili kupata pato halali.

Kupewa sadaka, kuokota au kuletewa zawadi. Njia hizi nazo sio endelevu na mwanaadamu hutakiwi kuyapanga maisha yake kwa kutegemea vyanzo vya mapato visivyo endelevu.

Kufanya kazi/ biashara

Bwana Mtume (Swallallaahu Alayhi Wasallam) ameisifu sana njia ya tatu ya kuhangaika kufanya kazi za kuajiri au kujiajiri ili kupata chumo la halali na akakemea sana mtu kuyapanga maisha yake kwa kuyaendesha kwa njia ya kuombaomba. Anasema:

“Hakutaacha kuombaomba kwa mmoja wenu mpaka atakutana na Mwenyezi Mungu ili hali hana katika uso wake hata kipande kimoja cha nyama”.

Mafunzo ya Uislamu yanamkemea mtu mvivu asiyependa kufanya kazi na anayepanga maisha yake ayaendeshe kwa njia ya kuombaomba labda kwa yule mwenye dharura ya msingi, mgonjwa asiyejiweza, mlemavu, aliyeharibikiwa na mambo yake ya uchumi.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation.

0 754 299 749

Advertisement