Ujenzi barabara Kigoma-Burundi wazinduliwa

Thursday July 18 2019

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Serikali ya Tanzania imezindua ujenzi wa barabara ya lami kutoka mkoani Kigoma kuelekea nchini Burundi yenye urefu wa kilomita 305.

Ujenzi wa barabara hiyo umezinduliwa leo Alhamisi Julai 18, 2019 na kaimu katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Khatibu Kazungu aliyebainisha kuwa ujenzi huo utatekelezwa kwa fedha za mkopo nafuu kutoka benki ya maendeleo ya Afrika.

Amesema  utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika nchi za maziwa makuu.

Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale amesema wamepokea Sh584.72 bilioni, kwamba mbali na barabara, fedha hizo zitatumika katika mradi wa elimu, afya pamoja na mradi wa maji.

Amesema ujenzi huo utaanza eneo la Kabingo wilayani Kakonko, Kasulu na Manyovu wilayani Buhigwe.

“Benki ya maendeleo ya Afrika imetukopesha fedha hizi  huku Serikali ya Tanzania ikichangia Sh58.7 bilioni  kwa mujibu wa mkataba tuliokubaliana,” amesema Mfugale.

Advertisement


Advertisement