Ujenzi wa Stigler’s Gorge walipiwa fedha za awali Sh688.65 bilioni

Muktasari:

Serikali imelipa fedha za awali kwa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme katika bonde la Mto Rufiji Stigler’s Gorge utakaofanyika kwa miezi 36 na kuzalisha umeme wa MW 2115

Dar es Salaam. Serikali imefanya malipo ya awali ya Sh688.65 bilioni kwa mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa kufua umeme katika bonde la Mto Rufiji, kampuni ya Arab Contractors.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya hundi yaliyofanyika leo Jumatano Aprili, 24 2019  jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amesema kiasi hicho cha fedha ni asilimia 70 ya kiasi cha asilimia 15 ya gharama za mradi zinazotakiwa kulipwa kama malipo ya awali.

James amesema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa kuwahi kutolewa na Serikali kama malipo ya awali.

Amemhakikishia mkandarasi kwamba fedha zipo na atalipwa kiasi chote cha Sh6.5 trilioni kama walivyokubaliaba kwenye mkataba.

Katibu mkuu huyo amebainisha kwamba malipo hayo yataendana na malipo mengine ambayo yatafanyika hivi karibuni.

Amesema kwa ujumla Serikali itakuwa imelipa Sh1 trilioni kama malipo ya awali kwa mkandarasi huyo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Hamis Mwinyimvua, amefafanua kwamba malipo ya awali ni asilimia 15 ya gharama ya mkataba ambayo imegawanywa katika sehemu mbili, asilimia 70 fedha za kigeni na asilimia 30 fedha za ndani.

Mwakilishi wa kampuni ya Arab Contractors, Mohammed Hassan ameishukuru Serikali kwa kutoa ushirikiano kwa kampuni yake ili mradi huo ufanyike kwa ubora na viwango vinavyotakiwa.