Ukaguzi maduka ya fedha watikisa Dar, mengi yafungwa

Muktasari:

  • Katika uchunguzi wake jana, Mwananchi ilishuhudia maduka kadhaa jijini Dar es Salaam yakiwa yamefungwa na hadi saa 6:00 mchana, maduka matatu tu maeneo ya Posta na matano Kariakoo ndiyo yaliyokuwa wazi.

Dar es Salaam. Katika muendelezo wa kudhibiti ubadilishaji holela wa fedha za kigeni, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jana ilifanya ukaguzi katika maduka ya fedha na kusababisha mengi kufungwa.

Jiji hilo linakuwa la pili baada ya ukaguzi kama huo kufanyika Arusha mwishoni mwa mwaka jana na kushuhudia maduka kadhaa yakifungwa kutokana na kukiuka sheria na mengine kutokidhi sifa zinazotakiwa.

Katika uchunguzi wake jana, Mwananchi ilishuhudia maduka kadhaa jijini Dar es Salaam yakiwa yamefungwa na hadi saa 6:00 mchana, maduka matatu tu maeneo ya Posta na matano Kariakoo ndiyo yaliyokuwa wazi.

Mmoja wa wamiliki wa maduka hayo anayefanya biashara zake eneo la Posta na ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema maofisa wa BoT wakiwa wameambatana na maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na maofisa wengine wa Serikali, walipita kukagua duka lake.

“Jana (juzi) walikuja hapa wakakagua mashine za EFD, kamera za CCTV na utendaji wetu wa kazi,” alisema.

“Waliniambia nifunge duka na watanipa majibu lakini hawajasema lini. Walichukua simu yangu na fedha.”

Mmoja wa wafanyabiashara aliye jirani na duka la Angola la Kariakoo, David Skaonga alisema aliona kundi la watu wakiingia kwa pamoja dukani kwake na baadaye walijitambulisha kuwa ni maofisa wa BoT na TRA wanafanya ukaguzi.

“Huu utaratibu wa kuvamia si mzuri. Waweke utaratibu wa kutoa elimu badala ya kushtukiza na kufunga maduka. Maduka haya yanatoa huduma muhimu kwa wafanyabiashara hapa Kariakoo,” alisema Skaonga.

Hatua hiyo inaweza kupunguza kasi ya biashara katika maeneo ya Kariakoo ambako wafanyabiashara, hasa wa nguo na vifaa vya kielektroniki hutegemea wateja kutoka nchi za jirani. Wafanyabiashara hao hutumia maduka hayo kubadilisha fedha na kuzitumia kufanya manunuzi kwa ajili ya kupeleka kwenye nchi zao, hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Zimbabwe.

Lakini taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa usimamizi wa benki na taasisi za fedha wa BoT, Jerry Sabi inaonyesha ukaguzi huo utaendelea na uwezekano wa maduka mengi zaidi kufungwa ni mkubwa.

Sabi amesema katika taarifa yake kuwa ukaguzi huo ulianza Februari 27 na umebaini maduka mengi ya fedha yanafanya biashara hiyo bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Sabi amesema kutokana na kilichobainika kwenye ukaguzi huo, BoT imeanza kutekeleza utaratibu wa kufuta leseni za maduka yanayokiuka masharti ya biashara hiyo na suala hilo bado linaendelea.

“Benki Kuu inapenda kuutahadharisha umma kutotumia huduma zisizo rasmi kubadilisha fedha za kigeni kutokana na hatari mbalimbali zilizopo ikiwamo kuibiwa au kupewa fedha bandia,” inasema taarifa hiyo.

“Aidha, utumiaji wa huduma zisizo rasmi ni kinyume cha sheria za nchi. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watoaji na watumiaji wa huduma zisizo halali.” Pia, imesema huduma hizo zinapatikana katika benki na taasisi zote za fedha pamoja na maduka ya fedha za kigeni ya Shirika la Posta Tanzania (TPC).

Hali kama hiyo ilijitokea pia kwenye ukaguzi mkoani Arusha uliofanyika Novemba mwaka jana ambako maduka 20 yalifungwa na kusababisha adha kwa watalii, wafanyabiashara na wasafiri katika mkoa huo maarufu kwa utalii nchini.