Ukawa ina fursa ya kung’ara zaidi 2015

Thursday November 13 2014

Wageni waalikwa na waandishi wa habari

Wageni waalikwa na waandishi wa habari wakisikiliza matokeo ya utafiti wa Twaweza kuhusu Tanzania kuelekea 2015, Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam Muungano wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) huenda ukapata nafasi kubwa katika Uchaguzi Mkuu 2015, utafiti mpya wa Taasisi ya Twaweza umebanisha.

Utafiti huo umebainisha kuwa kuungana kwa vyama hivyo kutaongeza ushindani na kukitisha Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kina ngome imara. Ukawa inaundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD.

Hata hivyo, takriban nusu ya Watanzania waliohojiwa katika utafiti huo uliowataka kubainisha iwapo upinzani ungesimamisha mgombea mmoja wangemchagua nani, walisema wangeichagua CCM na karibu theluthi moja wangemchagua mgombea wa upinzani iwapo watasimamisha mmoja.

Utafiti huo wa awamu ya 24 ulibainisha kuwa watu wawili kati ya 10 walikuwa tayari kumpigia mgombea badala ya chama wakati mmoja kati ya 10 akisema hajui angempigia nani iwapo upinzani ungemsimamisha mgombea mmoja 2015.

“Kundi lililosema kuwa wangemchagua mgombea wa upinzani lilipoulizwa kuwa nani anapaswa kuwa mgombea urais, watu wanne kati ya 10 (asilimia 41) walimtaja Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.

“Majina mengine ya viongozi wa upinzani yaliyopata zaidi ya asilimia 10 ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kwa asilimia 14 na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akipata asilimia kumi na moja.

Advertisement

Viongozi wengine wa upinzani waliotajwa kuwa wangefaa kugombea urais ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe kwa asilimia sita huku Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, wakiambulia asilimia moja kila mmoja.

Pamoja na mapendekezo hayo, bado karibu kila watu wawili kati ya 10 (asilimia 21) walioulizwa swali hilo walisema hawajui ni nani anafaa kugombea urais kupitia upinzani, jambo ambalo linaweza kubadili matokeo hayo kwa urais katika dakika za mwisho.

Advertisement