VIDEO: Ukikutwa na mfuko wa plastiki faini Sh30,000

VIDEO: Ukikutwa na mfuko wa plastiki faini Sh30,000

Dar es Salaam. Kama ulizoea kubeba kitu chochote kwenye mfuko wa plastiki ‘Rambo’ sasa kaa chonjo, ukikutwa unapigwa faini ya Sh 30,000.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema kuanzia Juni Mosi, mwaka huu mtu atakayekutwa amebeba mfuko wa plastiki adhabu yake itakuwa kulipa si chini ya faini ya Sh30,000.

Hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza bungeni jijini Dodoma kupiga marufuku uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia Juni Mosi ili kulinda mazingira.

Akizungumza jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Dar es Salaam, Waziri Makamba alisema sheria ya mazingira inamruhusu Waziri kutunga kanuni na tayari zimeshatungwa na zitaanza kutumika Juni Mosi.

Kanuni hizo pia zinataja adhabu kwa wanaoingiza mifuko hiyo ya faini ya Sh20 milioni au kifungo cha miaka miwili au vyote kwa pamoja. Kosa la kusafirisha nje ya nchi adhabu yake ni Sh5 milioni au kifungo cha miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Kosa la kuzalisha, kuhifadhi, kusambaza au kugawa adhabu yake ni Sh10 milioni au kifungo kisichopungua miaka miwili au vyote viwili, wakati kosa la kuuza adhabu yake si chini ya Sh100,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote kwa pamoja.

“Kukutwa na kutumia mifuko hiyo adhabu yake si chini ya Sh30,000,” inasema sehemu ya kanuni hizo.

Kifungu cha 5 cha kanuni hizo ambazo Mwananchi imeziona, kinasema mifuko yote ya plastiki bila kujali unene wake inazuiwa kuingizwa kutoka nje ya nchi au kusafirishwa, kuzalishwa, kuuzwa, kuhifadhiwa au kugawiwa na kutumika Tanzania Bara.

“Bila kukiuka kifungu cha kanuni cha 5, mtu hataruhusiwa kuuza, kutoa kwa ajili ya vinywaji au bidhaa yoyote inayouzwa kwa mifuko hiyo, labda kama aina ya bidhaa inalazimisha kufungashwa kwa plastiki,” kimesema kifungu cha 6.

Kifungu cha 7 cha kanuni hiyo kinasema baada ya kuanza kutumika kwa kanuni hizo, hakutakuwa na msajili au mtoa leseni au ruhusa kwa mtu yeyote anayetaka kuingiza mifuko hiyo, kusafirisha, kuzalisha au kuuza mifuko ya plastiki atakayeruhusiwa.

Akifafanua kuhusu katazo la kuzalisha na matumizi ya mifuko hiyo, Waziri Makamba alisema kwa zaidi ya miaka 15 Serikali imekuwa ikipambana bila mafanikio lakini kwa sasa wameamua kuchukua hatua ya mwisho. “Kuanzia mwaka 2003, baada ya 2006 ambapo zilichukuliwa hatua mbalimbali za kikodi, kodi ya plastiki iliwekwa hadi asilimia 120. kuna kipindi iliamulia mifuko yenye unene kuanzia micron 50 na ile myembamba izuiliwe.

SOMA:

Alisema zaidi ya nchi 60 duniani zimeshachukua hatua kali ya kupiga marufuku mifuko hiyo kutokana na athari za kimazingira, afya ya binadamu na wanyama.

“Katika dunia ya sasa ajenda kubwa ya mazingira ni matumizi ya plastiki. Kulikuwa na mkutano mkubwa wa mazingira mwaka juzi jijini Nairobi (Kenya) na kilichozungumzwa ni plastic pollution (uchafuzi wa plastiki) hasa kwenye bahari,” alisema.

“Taka zinapotupwa kwenye bahari zinaathiri sehemu nyingine. Kwa sasa asilimia 80 hadi 90 ya taka za baharini ni plastiki na utafiti unaonyesha ikifika mwaka 2050 taka za plastiki zitakuwa nyingi kuliko samaki.”

Akisisitiza kuhusu juhudi zilizochukuliwa na Serikali, Makamba alisema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani wamefanya juhudu mbalimbali hadi kufikia uamuzi mgumu wa kuzuia matumizi hayo.

“Tulianza kujifunza kwa nchi nyingine ikiwemo Zanzibar na kisha kukutana na wadau wakiwemo wenye viwanda na wazalishaji wa mifuko mbadala tangu mwaka 2016 na baada ya mkutano huo tukaamua Januari 1, 2017 tuanze kuzuia.

Soma:

Alisema Chama cha Wenye viwanda (CTI) na waagizaji waliomba katazo lianze Desemba 31, 2017 na wakati huohuo wakapewa maagizo ya kupambana kwanza na mifuko ya kufungashia pombe kali maarufu kama viroba.

“Jambo la viroba limeisha sasa tunaanza pale tulipoishia. tukaanza mazungumzo na wadau tena, tukakubaliana kwamba ni Juni Mosi, 2019,” alisema.

Alisema tayari kanuni zimeshatengenezwa zinazoeleza tafsiri ya mifuko ya plastiki, nini kinachokatazwa na muundo wa kitaasisi baada ya sheria.

Alitaja hatua nyingine kuwa ni kuundwa kwa kikosi cha kusimamia suala hilo na kwamba kuna taasisi 14 zitakazohusika.

Kuhusu uzalishaji wa mifuko mbadala, Waziri Makamba alisema Tanzania ina malighafi ya kutosha na tayari wadau wameonyesha nia ya kuanza kutegengeneza.

Huku akitoa mifano ya Rwanda na Kenya zilizopiga marufuku mifuko hiyo, alisema zinategemea malighafi kutoka Tanzania kutengeneza mifuko ya karatasi.

“Rwanda inasifika duniani kama mji msafi kabisa, lakini inawezeshwa na Tanzania. Kenya sehemu kubwa ya malighafi inatoka Tanzania. Kwa hiyo wanaopeleka malighafi wanatushangaa wakisema kuna malori na malori ya malighafi inakwenda nje,” alisema.

SOMA ZAIDI: