Ulega atangaza fursa mazao ya bahari Tanzania

Muktasari:

Tanzania imeweza kupambana na uvuvi haramu wa mabomu kwa zaidi ya asilimia 90 katika ukanda wa Pwani na kuweza kuingiza kiasi cha Sh 491 bilioni huku serikali ikipata mrabaha wa Sh15.8 bilioni kutokana na mazao ya bahari.

Lindi. Katika mwaka wa fedha ulioisha wa 2018/19 Tanzania ilifanikiwa kuuza jumla ya tani 38 milioni za samaki wa chakula nje ya nchi pamoja na samaki wa mapambo mmoja mmoja takribani pisi 40,000 waliogharimu kiasi cha Sh491 bilioni.

Pia, kutokana na mauzo hayo Serikali ya Tanzania ilifanikiwa kukusanya mrabaha wa Sh15.8 bilioni ikiwa ni matokeo chanya ya kupambana na uvuvi haramu wa mabomu kwa ukanda wa Pwani na kuweza kuongea pato la Taifa sambamba na kuinua hali ya wananchi.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Aguti 5, 2019 na Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega katika maonyesho ya nanenane kanda ya kusini yanayoendelea katika viwanja vya Ngongo.

“Mambo haya sio madogo yana uwezo mpana tukishikamana kwa pamoja kuliongezea pato la Taifa na kuinua hali za wananchi.”

“Mafanikio haya yanatokana na kudhibiti uvuvi haramu hasa wa mabomu na tumefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90 na nawapongeza wavuvi wote hasa wa ukanda wa Pwani walishirikiana na Serikali na wananchi kuhakikisha tunapambana na uvuvi huo,” amesema Ulega

Aidha amesema kutokana na mafanikio hayo viwanda vilivyokuwepo na kufa kutokana na ukosefu wa malighafi vimeanza kurejea ikiwemo kiwanda cha Abajuko Enterprises Limited  cha Mkuranga (mkoani Pwani) ambacho kina uwezo wa kuchakata takribani tani 2,000 huku akieleza kuwa oda za vyakula vya bahari kutoka nje ya Tanzania ni kubwa.

 

“Wale soko lao kubwa ni nje ya nchi na vilevile hapa ndani wanauza na vipo viwanda vingine baada ya uhakika wa malighafi na mkakati wetu wa kuhakikisha malighafi zinalindwa ni endelevu lakini ni shirikishi kwa sisi Serikali kushirikiana na wananchi ili kukuza uchumi,” amesema Ulega

Mjasiriamali wa mazao yatokanayo na bahari kwa ajili ya kutengeneza urembo mkoani Mtwara, Mkwamba Hassan amesema kwa miaka ya hivi karibuni upatikanaji wa malighafi umeanza kuwa rahisi baada ya uvuvi haramu hasa wa mabomu kudhibitiwa.

“Niipongeze Serikali na wadau wote tulioshirikiana kupambana na uvuvi haramu na kwa sisi wananchi wa ukanda wa Pwani tunaweza kuinua hali zetu za kiuchumi kama tutatumia vizuri fursa zilizopo na kuondolewa kwa changamoto zinazoweza kujitokeza,” amesema Hassan