Ulega awaongoza vijana kutoa damu kuwasaidia majeruhi ajali ya moto

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi akitoa damu kwa ajili ya kusaidia majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea eneo la Msamvu Mkoani Morogoro. Picha na Muyonga Jumanne

Muktasari:

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Abdallah Ulega amewaongoza vijana zaidi ya 50 wa Wilaya ya  Mkuranga kuchangia damu kwa ajili ya majeruhi wa ajali ya moto  waliolazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Abdallah Ulega amewaongoza vijana zaidi ya 50 wa Wilaya ya  Mkuranga kuchangia damu kwa ajili ya majeruhi wa ajali ya moto  waliolazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Ajali hiyo ilitokea Jumamosi Agosti 10, 2019 katika mtaa wa Itingi, Msamvu barabara ya Morogoro-Dar es Salaam baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.

Hadi sasa watu 76 wamekufa huku wengine zaidi ya 50 wakiendelea kupatiwa matibabu MNH na hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Ulega amesema damu inahitajika nyingi kwa ajili ya majeruhi, kuwataka watu wa kada mbalimbali kuchangia..

“Kama kiongozi najua kuna tatizo kubwa la damu nchini kwetu, hata wilayani kwangu pale Mkuranga na hospitali zote, ni jambo jema uwepo utaratibu wa kutoa damu kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu", amesema Ulega.

Neema Maro, mfanyakazi wa kitengo cha damu salama amesema uhitaji wa damu ni mkubwa na kuwaomba wananchi, taasisi za kiraia na kidini kuchangia damu.

"Tangu majeruhi waletwe hapa tulipata chupa 70 kutoka kwa kamanda wa polisi mstaafu, Suleiman Kova akiwa na kikundi cha Jogging cha Temeke na jana pia walikuja waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ushirika wa Kinondoni na siku zinavyokwenda tunaona vijana na watu wengi wanakuja na leo ni Ulega,” amesema.