VIDEO: Ulimwengu: Kuogopa kufa ukitetea haki ni ujinga

Muasisi wa Kampeni ya ChangeTanzania, Maria Sarungi akibadilishana mawazo na Mwanahabari Mkongwe, Jenerali Ulimwengu (katikati) pamoja na Mchora Katuni, Masoud Ally wakati wa mjadala kuhusu haki na wajibu wa rai ulifanyika jijini Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Mwandishi mkongwe, Jenerali Ulimwengu amesema kuogopa kufa kwa sababu ya kutetea haki ni ujinga huku akidai kwamba ni bora kufa kwa kutetea jambo la haki kuliko kufa kwa ugoni na mambo ya kipuuzi

Dar es salaam. Mwandishi mkongwe, Jenerali Ulimwengu amesema kuogopa kufa kwa sababu ya kutetea haki ni ujinga.

Amesema kila Mtanzania atakufa bila kujali sababu akibainisha kuwa ni suala la muda tu.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Februari 20, 2019 katika kongamano la  "Wenye Nchi ni wananchi' lililoandaliwa na Jukwaa la Change Tanzania.

"Kuogopa kufa ni ujinga, bora kufa kwa kutetea jambo la maana kuliko kufa kwa ugoni au mambo ya upuuzi," amesema nguli huyo wa habari wakati akitoa rai kwa wanaoogopa kuzungumza ukweli kuhusu hali ya demokrasia nchini.

Msingi wa kauli hiyo alikuwa akieleza dhana ya uthubutu kwa vijana, akifafanua dhana ya uwajibikaji katika hatua ya ushiriki wa maendeleo na ulinzi wa Katiba ya nchi kwa kuhoji mambo yanayokwenda kinyume. 

"Humu tuko Wangapi? (ukumbini), nawatangazia rasmi wote tutakufa, watanzania wote milioni 57 watakufa kwa hiyo jambo la muhimu ni kuwa waaminifu zaidi kuliko kuwa watii, kataa amri isiyo halali, isiyo ya haki na tenda mema.’’

Alitolea mifano ya wateule wanaotumia kigezo cha kutekeleza maagizo ya kutoka juu bila kujali athari zake.

Pamoja na kauli hiyo, Jenerali amewafundisha vijana walioshiriki jukwaa hilo kutetea mtu usiyemjua, mnyonge, kuwa mwaminifu zaidi ya kuwa mtiifu, kushiriki katika maendeleo ya Tanzania, kukemea maovu na kutenda mema wakati wote.

Amesisitiza dhana ya uanaharakati siyo kukosa kazi, kuwa mchochezi bali ni uhai na ndiyo inayoendesha harakati za mabadiliko chanya katika jamii.

Katika hatua nyingine amewataka wananchi na viongozi nchini kutenda haki kama watatakavyo watu wengine wawatendee wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa hilo, Maria Sarungi amesema jukwaa hilo linaunganisha vijana kutafakari na kujengea maarifa juu ya haki na wajibu wao kwa Taifa badala ya kuwaachia wanasiasa kuwa na hakimiliki ya kuwaamulia mabadiliko wanayoyataka.

Amesema jukwaa hilo lililoanza mwaka 2012, lina lengo pia la kuelimisha na kusaidia wanachama wake watakaoathirika na sheria ya makosa ya mitandaoni, kukumbusha wajibu wao wa msingi na kuimarisha mtandao wa uanaharakati katika mabadiliko chanya.

Annastazia Rugaba kutoka taasisi ya Twaweza amesema anatamani kuona vijana wakijengewa uwezo na fikra mpya za kutambua wajibu wao kwa Taifa badala ya kuonekana walalamikaji mitandaoni, wakidai haki zao za msingi au kukosoa uwajibikaji wa viongozi pekee.