VIDEO: Ulinzi waimarishwa kesi za Mbowe, CUF

Muktasari:

  • Leo Jumatatu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutakuwa na kesi mbili zinazohusisha viongozi wa  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF)

Dar es Salaam. Hali ya ulinzi umeimarishwa katika Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

Ulinzi huo unatokana na kesi mbili tofauti kusikilizwa leo Jumatatu Februari 18, 2019 katika mahakama hizo kwa nyakati tofauti.

Katika Mahakama ya Rufaa, inatarajia kusikilizwa rufaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) dhidi Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Esther Matiko.

DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, kukubali kuendelea na usikilizwaji wa rufaa ya wabunge hao ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu kuwafutia dhamana.

Wakati hayo yakitarajia kujiri hapo, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambayo ipo karibu mita 100 kutoka Mahakama ya Rufaa, kutasikilizwa uamuzi wa ipi bodi halali ya Chama cha Wananchi (CUF).

Ni ama kambi ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba ama kambi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Moja kati ya kambi hizo itatoka mahakamani huku ikiwa na furaha na nyingine ikiwa na huzuni ama machungu, baada ya Mahakama Kuu kubainisha wajumbe halali wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kati ya makundi mawili ya wajumbe yanayovutana.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa leo na Jaji Dk. Benhajj Masoud wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakati atakapotoa uamuzi wa kesi inayohusu mgogoro wa wajumbe halali wa bodi ya wadhamini wa chama hicho.

Mwananchi  ambalo limeweka kambi katika mahakama hizo limeshuhudia magari ya polisi likiwemo la maji ya kuwasha yakiwa yameegeshwa pembezoni mwa mahakama hizo huku polisi wenyewe silaha wakifanya doria za kutembea huku na kule kuimarisha ulinzi.

Polisi imezuia watu kupita pembezoni mwa Mahakama ya Rufani badala yake imewataka wapite ng'ambo ya pili.

Mwananchi imeshuhudia baadhi ya watu kuzuiwa kupita eneo hilo na kuamriwa kupita sehemu nyingine.

Pia kuna ukaguzi maalumu katika lango la kuingilia Mahakama ya Rufani.

Vivyo hivyo hali hiyo ipo katika Mahakama ya Kuu

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachojiri