Ummy, Kangi kushiriki mazishi ya watu 15 walioteketea kwa moto ajali ya Hiace Mara
Muktasari:
- Mawaziri Ummy Mwalimu na Kangi Lugola wanatarajiwa kuungana na wakazi wa wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara leo katika mazishi ya watu waliofariki katika ajali iliyohusisha magari mawili ya abiria na kuungua moto
Tarime. Mawaziri wawili wanatarajiwa kushiriki mazishi ya watu 15 kati ya 16 waliofariki kwenye ajali iliyohusisha magari mawili ya abiria katika kijiji cha Komaswa wilayani Tarime mkoa wa Mara Jumatatu iliyopita.
Mawaziri hao ni ni wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Ummy Mwalimu ambaye tayari amefika mkoani Mara na Kangi Lugola wa mambo ya ndani ambaye anatarajiwa kuwasili wakati wowote kuanzia sasa.
Watu hao walifariki baada ya magari madogo ya abiria ‘Hiace’ yanayofanya safari zake kati ya Musoma -Tarime na Tarime- Busurwa wilayani Rorya kugongana uso kwa uso na kisha kulipuka moto.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema tayari maandalizi yamekwisha fanyika ikiwa ni pamoja na kuchimbwa makaburi na majeneza kwa ajili ha mazishi.
Wengine wanaotarajiwa kushiriki ni wakuu wa wilaya za mkoa wa Mara pamoja na viongozi mbalimbali wa kisiasa.
Katika ajali hiyo watu 15 walifariki papo hapo huku wengine wanne wakinusurika ingawa mmoja alifariki njiani wakati wakipelekwa hospitalini.
Endelea kufuatilia Mwananchi